Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati yashauri mambo saba suala la korosho

40296 Pic+korosho Kamati yashauri mambo saba suala la korosho

Wed, 6 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji imetaja mambo saba katika kukabiliana na changamoto za zao la korosho ikiwamo uhakiki wa uwazi unaowashirikisha wakulima wenyewe au vyama vyao vya ushirika na masoko.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamoud Mgimwa akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo jana alisema operesheni ya korosho inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo kuchelewa kwa malipo ya wakulima.

Changamoto nyingine ni uwezo mdogo wa viwanda vya ndani kubangua korosho iliyovunwa, uwezo mdogo wa ghala kuu la kuhifadhia korosho, kuchelewa kulipwa kwa malipo ya halmashauri na vyama vya msingi.

“Kushuka kwa mapato ya fedha za kigeni na kukosekana kwa Bodi ya Korosho Tanzania hivyo kupelekea ugumu wa utekelezaji wa operesheni nzima,” Mgimwa aliitaja kuwa ni sababu nyingine.

Mbunge huyo wa Kalenga (CCM), alisema kuteuliwa kwa Bodi hiyo mapema iwezekanavyo kutasaidia utekelezaji wa majukumu yanayohusu zao hilo badala ya ilivyo sasa ambako yanatekelezwa na bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko iliyo na majukumu yake kimsingi.

“Ili kudhibiti mazingira ya rushwa kutokana na kuchelewa kwa kazi ya uhakiki wa malipo ya wakulima, ni vyema uhakiki ukakamilika mapema iwezekanavyo,” alisema.

Maoni hayo ya kamati yamekuja wakati hivi karibuni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wadau wa korosho aliagiza mamlaka zinazohusika kuhakikisha kwamba hadi jana, uhakiki unakamilika na malipo yakamilike kabla ya Februari 15.

Kuhusu ulipaji wa fedha za korosho kwa wakulima, Mgomwa alitaka uende sambamba na malipo ya ushuru wa halmashauri ili kuziongezea uwezo wa mapato ya ndani kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.

Pia, kamati hiyo ilitaja jambo jingine kuwa ni minada ya korosho kufunguliwa mapema kwenye maeneo ambayo korosho inawahi kukomaa ili kudhibiti walanguzi maarufu kama kangomba.

Alisema kamati yake pia imeshauri Serikali kuandaa mkakati wa muda mrefu utakaoshughulikia changamoto za masoko kwa mazao yote.

Katika mchango wake, mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia alisema muda unaotambuliwa wa ununuzi wa korosho kwa wakulima kwa kawaida huanza Oktoba hadi Desemba.

“Sasa hivi hadi Februari hata asilimia 60 ya ununuzi haijafikiwa, uhakiki wamehakiki zaidi ya tani 200,000 lakini wanaolipwa hata haijafikiwa tani 150,000,” alisema.

Lakini cha kushangaza, alisema takwimu zinaonyesha kwamba kati ya vyama vya ushirika 605 wameshalipa 600.

Alisema hadi jana wakulima wakubwa hawajalipwa jambo ambalo limekuwa kama adhabu.



Chanzo: mwananchi.co.tz