Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati yahoji kupungua utafiti, uwekezaji sekta ya mafuta na gesi

9544 Kamati+pic TZWeb

Wed, 20 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Kamati ya Bajeti imewasilisha taarifa yake bungeni yenye zaidi ya mambo 20, ikizungumzia pia kupungua kwa utafiti na uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi.

Taarifa hiyo kuhusu hali ya uchumi, Mpango wa Taifa wa Maendeleo na bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 iliwasilishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Ghasia.

Ghasia alisema takwimu zinaonyesha shughuli za utafutaji na uwekezaji katika mafuta na gesi zimekuwa zikipungua siku hadi siku, hivyo kushindwa kukidhi matarajio ya Serikali katika sekta hiyo kuweza kuchangia bajeti ya Serikali.

“Hivi karibuni tumeshuhudia kampuni kubwa ya Marekani ya Exxon Mobil ikionyesha nia ya kuuza visima vyake vya gesi nchini licha ya kuwa ilianza mchakato wa kuwekeza kwa njia ya kuchangia mtaji katika mradi wa LNG Likongo mkoani Lindi,” alisema.

Alisema Serikali haijaeleza mkakati wowote uliopo wa kuhakikisha inapata mapato yatokanayo na shughuli za utafutaji na uwekezaji wa mafuta na gesi.

“Taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2017 imeshindwa kuchambua hali ya maendeleo katika sekta ya mafuta na gesi,” alisema.

Ghasia alisema kamati inaishauri Serikali kufanya tafiti na kuona nini hasa kimechangia kupungua kwa shughuli za utafutaji mafuta na gesi, na nini kifanyike kwa haraka kurekebisha kasoro hiyo.

Alisema sura ya bajeti inatakiwa kuonyesha kiasi cha mapato yaliyopatikana kwenye utafutaji na uwekezaji wa mafuta na gesi.

Deni la Taifa

Kamati hiyo imetoa angalizo kuwa masharti ya mikopo yazingatiwe uhimilivu wa deni la Serikali na fedha za mikopo zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo ambayo itachochea ukuaji wa uchumi.

Alisema deni la Taifa la Sh10 trilioni bado linachukua asilimia 30 ya bajeti yote ya Serikali na asilimia 49 ni matumizi ya kawaida.

Alisema mishahara iliyotengewa Sh7.3 trilioni inachukua asilimia 36 ya matumizi ya kawaida na matumizi mengineyo Sh3.9 trilioni yanachukua asilimia 15 ya matumizi ya kawaida.

Ghasia alisema changamoto iliyopo ni katika deni la Taifa na mishahara ambayo imechukua Sh17.3 trilioni sawa na asilimia 53 ya bajeti yote.

“Huu sio uwiano mzuri hata kidogo kwa utekelezaji wa bajeti ya Serikali,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema ingawa deni hilo haliepukiki, lakini ni mzigo mkubwa katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa kuwa linaathiri upatikanaji wa fedha za matumizi mengine (OC) kwa mafungu mbalimbali.

Alisema jitihada zinahitajika ili kuhakikisha ulipaji mkubwa wa deni la Taifa unapungua.

Kodi ya Vat

Alisema kuondolewa kodi ya ongezeko la thamani (Vat) kwenye taulo za usafi kike hakutakuwa na manufaa kwenye mabadiliko ya bei.

Kamati imesema hatua hiyo itawafanya wazalishaji wa ndani kushindwa kurejeshewa kodi hiyo waliyolipia katika malighafi walizotumia.

Alisema msamaha utawanufaisha zaidi wazalishaji wa nje wanaoleta bidhaa hiyo nchini kuliko wazalishaji wa ndani.

“Kamati inashauri Serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya Vat sura 148 kifungu cha (6) ili kutoa fursa ya wazalishaji wa ndani kurejeshewa VAT watakazokuwa wamelipa wakati wa ununuzi wa malighafi,” alisema.

Misaada na mikopo

Alisema Serikali katika bajeti imesema inatarajia kupata Sh2.67 trilioni kutoka kwenye misaada na mikopo ya nje ya nchi.

Ghasia alisema kiasi hicho ni pungufu ya asilimia 32.5 kulinganisha na bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2017/18 ilipokuwa Sh3.9 trilioni.

Kuhusu mikopo ya masharti ya kibiashara kutoka nje, alisema Serikali imepanga kukopa Sh3.11 trilioni sawa na ongezeko la asilimia 95 kulinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18.

“Kamati inajiuliza upungufu huu mkubwa wa mikopo na misaada kutoka nje unatokana na nini? Je ni Serikali kujizatiti kimapato? Au ni kwa sababu Serikali haikidhi vigezo na masharti ya kupata misaada na mikopo ya masharti nafuu?” alihoji.

Alisema kama ni hivyo, ni juhudi gani zinafanywa ili kufikia viwango na vigezo hivyo vya mikopo na misaada kwa ajili ya mwaka 2018/19.

Kuhusu ushuru

Kamati imesema pendekezo la Serikali kuingiza makusanyo ya ushuru katika mfuko mkuu wa Serikali, litakuwa ni msumari wa mwisho kwenye jeneza la mazao ya biashara ya korosho, karafuu, katani, chai, tumbaku, pamba na kahawa.

Alisema kamati inashauri Serikali kuendelea kuziachia bodi zote za mazao fedha zinazokusanywa kutoka kwa wakulima kwa ajili ya uendelezaji wake na si vinginevyo.

Kamati imesema mwenendo wa kutoa fedha za maendeleo ambao ni chini ya bajeti ya maendeleo iliyoidhinishwa unaonyesha kwa namna gani Serikali imeshindwa kuendana na malengo yake ya kuhakikisha miradi inatekelezwa kama ilivyopangwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz