Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati yaguswa changamoto sekta ya chuma

C8c3bd28f8f78a40b92da9c2e8f2933d Kamati yaguswa changamoto sekta ya chuma

Thu, 28 Apr 2022 Chanzo: Habarileo

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, imeahidi kushugulikia kero zinazoikabili sekta ya chuma nchini, ili kuhakikisha Tanzania yenye viwanda inapiga hatua zaidi.

Ahadi hiyo ilitolewa juzi wakati wa ziara katika viwanda vya Alaf na MMI Steel, ambavyo vinavyozalisha mabati ya chapa ya Simba Dumu na Kiboko.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, David Kihenzile alisema hiyo ilikuwa moja ya ziara za kawaida za kamati hiyo, ambapo wajumbe walipata nafasi ya kujifunza mengi kuhusu sekta ya chuma.

“Kupitia ziara hii tumepokea changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya chuma kutoka kwa viwanda hivi vya Alaf na MMI Steel na kama kamati tumekubaliana kimsingi kuwa changamoto hizi zinatakiwa kufanyiwa kazi kwa hivyo tumezipokea na tunaenda tutazishugulikia,” amesema.

Amesema moja ya malengo ya kamati hiyo ni kuhakikisha kuwa viwanda vya ndani vinafanya shughili zake bila vikwazo, na watajitahidi kuhakikisha serikali inatatua baadhi ya changamoto hizo kama sio zote.

Amesema baadhi ya changamoto zilizoainishwa na Alaf na MMI Steel ni pamoja na, kuwepo baadhi ya wawekezaji wanaoagiza bidhaa ambazo ni za viwango vya chini, ushindani mdogo na viwanda vingine katika ukanda wa Afrika Mashariki, ukadiriaji wa chini wa kodi kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje, waagizaji kutoka nje kujiita wazalishaji, ucheleweshaji wa VAT refund, bidhaa bandia sokoni na madhara ya UVIKO-19.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, kamati yake itaangalia namna ya kuishauri serikali kuweka mazingira sawa ya biashara, ili kuhakikisha ushindani sawa na sio hali hii ya sasa hivi, ambapo wawekezaji wa ndani wanawekeza fedha nyingi huku wafanyabiashara wengine wakiagiza kutoka nje na kupenya katika soko la ndani bila shida yoyote.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Alaf Tanzania, Ashish Mystry amesema ziara ya kamati hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa na inadhihirisha kuwa serikali inaijali sekta ya uzalishaji.

“Nina uhakika kamati hii itatusaidia kupata suluhisho ya changamoto zinazokabili sekta ya chuma nchini,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa MMI Steel, Patel Veer amesema wana nia ya kuendelea kuwekeza zaidi hasa serikali ikiahidi kushugulikia changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa sasa.

“Uwekezaji tuliofanya hadi sasa ni mkubwa sana tunaiomba serikali itulinde dhidi ya wafanya biashara ambao wanaingiza bidhaa za viwango vya chini kiholela na wanaweza kukabiliana na hali hii kwa kuwatoza kodi kubwa,” amesema.

Chanzo: Habarileo