Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefanya ziara ya kutembelea Mradi wa Bomba la Mafuta uliopo Chongoleani ili kukagua maendeleo ya Mradi huo kutoka Hoima Nchini Uganda hadi Tanga.
Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo hilo la Chongoleani Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini Mhe. David Mathayo amesema kuwa Kamati imeridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa na Mradi huo na wanamatumaini makubwa utakamikika kwa wakati
"Tumefurahishwa sana na maendeleo ya hatua yaliyofikiwa na Mradi huu tuneona wako mbele zaidi katika utekelezaji wake," alisema Mathayo.
Aidha mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini David Mathayo amesema Mradi huo ni muhimu kwa watanzania kwa kuwa utaleta manufaa makubwa kwa nchi.
"Tunafahamu kuwa watu wanausema vibaya Mradi huu ila sisi wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunasema huu mradi ni muhimu sana kwetu na uendelee kwa kuwa hauna madhara yoyote na una manufaa makubwa kiuchumi" aliongeza Mathayo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Athumani Mkutuka amesema Serikali imepokea maelekezo pamoja na ushauri uliotolewa na Kamati hiyo na watahakikisha miradi yote mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali wanatimimiza jukumu la kurudisha sehemu ya faida kwa jamii ili waweze kunufaika na uwepo wa miradi hiyo.
Aidha, Kamati ya bunge imetoa maoni Yao kuhusu suala la kuisaidia jamii kuwa watekelezaji wa Mradi huo waangalie kwa mapana zaidi namna ya kuendelea kuisaidia jamii inayowazunguka.