Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imesema haijaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme katika vijiji 78 vya wilaya tatu mkoani hapa inayotekelezwa na mkandarasi wa Kampuni ya TONTAN Electricity Company Limited na kuiagiza Wizara na Serikali Mkoa kufuatili mwenendo wake.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dunstan Kitandula ametoa msimamo huo leo wakati akiitambulisha kamati yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba.
Amesema kamati hiyo iliwasili jana Jumatano na kukagua utekelezaji wa miradi ya ufikishaji umeme vijijini REA katika Wilaya za Korogwe Mkinga na Pangani ambapo licha ya kuwa muda wa kukamilika muda wa mkataba, lakini hadi jana ni vijiji tisa pekee vilivyopata umeme kati ya 78 ilivyokabidhiwa.
Amesema Wilaya ya Korogwe mkandarasi huyo alimekabishiwa vijiji 54 lakini hadi jana vilivyopata umeme vilikuwa vinne pekee, Mkinga alipewa vijiji 22 alivyofikisha umeme ni vinne na pangani kijiji kimoja kati ya viwili.
"Kamati haijaridhika na kasi ya utekelezaji wa mradi wa ufikishaji umeme vijijini REA unaotekelezwa na mkandarasi TONTAN tumeshaielekeza Wizara ya Nishati lakini tunamkabidhi pia kwa Serikali Mkoa kwa ajili ya ufuatiliaji mwenendo wake," amesema Kitandula.
Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amekiri kuwa kasi ya mkandarasi huyo haiwaridhishi kwa kuwa mkataba wake unaisha mwezi Agosti 2023 na hadi sasa hajafikia asilimia 70 ya utekelezaji.