Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati ya Bunge yaridhishwa uhakika umeme wa gesi

Mgawo Wa Umeme No Kamati ya Bunge yaridhishwa uhakika umeme wa gesi

Thu, 13 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na uhakika wa upatikanaji wa umeme wa gesi katika kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi II ambacho kinazalisha megawati 240 ambazo zinaingizwa kwenye gridi ya taifa.

Kamati hiyo imefanya ziara katika Kituo cha Kinyerezi II kujionea uendeshaji wake, kabla ya kutembelea kituo hicho, kamati ilitembelea mitambo ya uzalishaji wa gesi mkoani Mtwara.

Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 13, 2022 baada ya kukagua shughuli zinazofanyika, mwenyekiti wa kamati hiyo, Dunstan Kitandula amesema wameona jinsi kituo hicho kinavyoweza kuzalisha megawati 240 na upatikanaji wake ni stahimilivu.

"Tanesco wametuhakikishia wana mipango madhubuti ya kuhakikisha wana uwezo wa kupata vifaa kipindi chote cha mwaka bila kuwa na matatizo yoyote," amesema Kitandula.

Mwenyekiti huyo amesema wamefurahi kuona kituo hicho kinaendeshwa na Watanzania wenyewe, jambo ambalo amesema ni zuri kwa mustakabali wa taifa hili.

"Kwa niaba ya kamati, tunaipongeza serikali kuona umuhimu wa kuweka macho yake kwenye eneo hili ambalo ni muhimu sana siyo tu kwa kupata umeme lakini pia katika kukuza uchumi.

"Tuendelee kufanya kazi kwa ufanisi ili kuhakikisha kwamba nchi yetu haiingii kwenye matatizo ya kukosa umeme," amesema Kitandula.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco (Usambazaji), Atanasius Nangali amesema kituo cha Kinyerezi II kinafanya kazi kwa asilimia 100 na kamati imekuta mashine zote nane zinafanya kazi ya kufua umeme.

"Wataalamu wote wanaokiendesha kituo hiki kwa asilimia 100 ni wataalamu wa Kitanzania. Serikali inatupa support (msaada) kubwa katika uzalishaji wa umeme katika vyanzo vyetu mbalimbali," amesema Nangali.

Chanzo: mwanachidigital