Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati ya Bunge yakerwa na deni, uendeshaji ATCL

NDEGE 1?fit=800%2C450&ssl=1 Air Tanzania

Tue, 31 Aug 2021 Chanzo: Mwananchi

Dodoma, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imekataa kupokea hesabu za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), huku ikihofia kufa kwake endapo Serikali haitachukua hatua za makusudi za kulinusuru.

PAC imeagiza kufanyike kikao cha pamoja kati ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ofisi ya Rais, Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) na Shirika hilo.

Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akizungumza na Mwananchi baada ya kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka unaoishia Juni mwaka 2019/2020 ya shirika hilo.

Amesema jambo kubwa walilobaini baada ya kuchambua vitabu hivyo vya CAG ni kampuni hiyo kuwa na mtaji hasi wa Sh216.6 bilioni ambao unatokana na ATCL kuwa na madeni ya Sh472.8 bilioni wakati thamani ya mali zake ni Sh256.2 bilioni.

“Shirika likiwa na mtaji hasi ina maana hapo linakuwa kama limekufa kwa kanuni yetu (kihasibu) ya ‘going concern’ tunasema tuna wasiwasi kuwa hili halipo, haliwezi kuendelea kuwepo,” amesema Kaboyoka.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Japhet Hasunga amesema miongoni mwa mambo yaliyochangia ATCL kuwa na mtaji hasi ni deni la Sh138 bilioni (sawa na dola za Marekani milioni 60) lililokuwa likidaiwa baada ya kampuni ya Wallis Trading iliyolikodisha ndege (A320-214) kushinda kesi mahakamani.

“Kwanza kuna hoja nyingi za kiukaguzi hazijajibiwa kikamilifu, lakini hawakuweza kufikia malengo ya kibiashara. Walikuwa na matarajio ya kupata zaidi ya Sh600 bilioni lakini wamepata Sh157 bilioni tu sawa na asilimia 24 ya malengo yao,” amesema.

Hasunga alipoulizwa ATCL walitoa sababu sababu gani zilizowafanya wasifikie malengo hayo, alisema walidai kuwa ugonjwa wa Uviko-19 lakini wao (PAC) wamebaini sababu nyingine ambazo zimelifanya kutofikia lengo.

Hasunga amesema kamati inaona miongoni mwa sababu ni ruti nyingi kutofanyiwa kazi na zilizopo kutosimamiwa ipasavyo.

Ametoa mfano wa malalamiko makubwa ya wateja kuwa wanaahirisha safari zao na uchelewaji wa ndege zao.

Amesema pia wamebaini kuwa bodi hiyo imeshindwa kufanya usuluhishi wa madeni ambapo kuna deni la Sh4.4 bilioni halijafanyiwa usuluhishi.

Lakini, Hasunga amesema bodi hiyo imeshindwa kukusanya madeni ya Sh4.7 bilioni ambayo wanawadai wateja mbalimbali.

Pia, amesema kuna malipo ya Sh1.5 bilioni yalifanywa na Kampuni hiyo bila kuzingatia utaratibu ikipata hasara ya Sh60.2 bilioni katika mwaka huo wa fedha.

Makamu Mwenyekiti huyo amesema wamebaini kuwa bodi hiyo imezipa kazi kampuni zinazotoa huduma mbalimbali zenye thamani ya Sh4.8 bilioni bila kuwa na mkataba.

Mwananchi lilimtafuta Mwenyekiti wa wa Bodi ya ATCL, Emmanuel Korosso na kumuuliza kuhusu hatua hiyo, lakini alisema: “Kwanza hizo taarifa siyo sahihi, pili siruhusiwi kutoa taarifa za PAC.”amesema

PAC pia walikataa kupokea hesabu za ATCL kutokana na mtatizo ya kampuni hiyo.

Hasunga amesema shirika hilo linataka ndege ziwe chini yao ili ziwe sehemu ya mtaji wao lakini kamati hawakubaliani na kuhamisha umiliki huo.

“Wao wanasema sababu zilizokuwa zinatajwa ni wamalize deni na deni lilishaisha lakini sisi tunasema wangekopa benki si wangelipa mkopo na riba. Sasa hapa (kwa wakala ) ni sawa sawa umekopeshwa unatakiwa kulipa mkopo na riba wao hawataki,” amesema.

“Kuna mtaji mkubwa uliotolewa na Serikali lakini bado nchi haitaweza kuona manufaa yake inayotarajia…Kuna ndege nyingine zinakuja watu wenyewe ukiwaangalia hawawezi kufanya kazi,” amesema.

Hasunga amesema walikuwa wafanye kikao na TGFA, lakini hakikufanyika baada ya ofisa masuhuli kutofika bila taarifa

“Badala yake (Ofisa masuhuli) akaleta ofisa mdogo sana anayekaimu ambaye asingeweza kujibu maswali (ya wajumbe wa kamati) wangeuliza,”amesema.

Pia, amesema watendaji wote wa wakala huo wanakaimu nafasi zao kwa hivyo waliona kuwa Bunge haliwezi kuwashauri makaimu wala kuwapa maagizo.

“Tuliwaambia waende wakajipange waje na ofisa masuhuli (Katibu mkuu wa wizara husika) waje wajibu maswali. Tunataka kuongea na watu wanaohusika kwa mujibu wa kanuni za Bunge na si watu wasiotajwa katika kanuni za Bunge,” amesema.

Amesema hatua hiyo inaonyesha kuwa wakala huyo hawajatoa uzito unaostahili suala hilo.

Chanzo: Mwananchi