Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati ya Bunge yaitaka Serikali kuurejeshea mgodi Sh11 bilioni

Pic Fedha Data Wastaafu Kamati ya Bunge yaitaka Serikali kuurejeshea mgodi Sh11 bilioni

Fri, 23 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imeitaka Serikali kuurejeshea Mgodi wa Stamigold Sh11 bilioni zinazotokana na kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

Lengo ni kutaka kuuwezesha mgodi huo kuendelea kujiendesha na kulipa madeni unayodaiwa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deus Sangu amesema hayo leo Alhamisi Februari 22, 2024 wakati kamati hiyo ilipoutembelea mgodi huo.

Sangu amesema Bunge lililopita liliielekeza Serikali kurejesha VAT yote inayodaiwa na mgodi huo inayofikia Sh11 bilioni.

“Kamati hii sisi tunawalea na tunajali uwekezaji, mara ya mwisho kuja hapa mlikuwa na changamoto kubwa ya umeme, kupitia kamati hii tumesogeza jambo hilo na baadaye mmepata umeme na sasa mmeondoa gharama ya Sh1 bilioni mliyokua mkilipa kila mwezi. Na leo tunafanya ziara hapa ili kuona yale tuliyojadili Dodoma na utekelezaji wake unaendaje,” amesema Sangu.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk Venance Mwasse alisema mafanikio makubwa ya mgodi huo yametokana na mpango kazi waliojiwekea pamoja na ushirikiano wa watumsihi na viongozi, ambao walifanikiwa kuufufua mgodi uliokuwa ufungwe mwaka 2017.

“Tulikaa chini tukaweka mipango, Serikali ilishaamua kuufunga mgodi na hata Rita (Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini walikua wameshaambiwa waje kwa ajili ya kufilisi, lakini mwaka 2018 tukalipa madeni ya watumsihi na kupunguza madeni mengine na mimi nilipoingia hapa, nilikuta la Sh63 bilioni,” amesema.

Amesema kama mgodi huo ungekufa, wafanyakazi zaidi ya 600 wangekosa ajira, lakini hivi sasa wanaendelea na ajira na wamefanikiwa kulipa mapato serikalini na kuendelea kupunguza madeni wanayodaiwa.

Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Ally Ally amesema lengo la marekebisho ya sheria ya VAT ilikua ni kuwawezesha wachimbaji wauze dhahabu hapa nchini pamoja na kuhakikisha madini yanaongezewa thamani kabla ya kusafirishwa kwenda nje.

Lakini amesema hali kwa sasa ni tofauti,…“Tunauza dhahabu nje ya nchi na VAT inakuwa ‘zero rated’.”

Ameshauri ili kuondoa changamoto hiyo anashauri Serikali iiondoe kodi ya VAT kwenye uchenjuaji na kuhamishiwa katika vipengele vinavyohusika na ununuzi wa vifaa, ili isaidie mgodi kufikia lengo la kuongeza thamani ya madini hapa nchini.

Akizungumzia mafanikio ya mgodi huo, Ally amesema kuunganishwa kwa nishati ya umeme kumepunguza gharama za uendeshaji na kuokoa zaidi ya Sh700 milioni kwa mwezi.

Amesema mgodi huo pia umefanikiwa kulipa Sh21.52 bilioni kutoka kwenye mapato ya ndani na kupunguza madeni yaliyokuwepo ya Sh47.3 bilioni mwaka 2022.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live