Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeitaka Serikali kukiangalia kwa jicho la tofauti kiwanda cha kutengeneza mashine na kuzalisha vipuri cha Kilimanjaro (KMTC) ili kukiwezesha kufanya kazi kikamilifu na kurahisisha upatikanaji wa vifaa mbalimbali.
Kiwanda hicho kilichosimamisha uzalishaji wake kwa zaidi ya miaka 30, tayari Serikali imewekeza zaidi ya Sh4 bilioni, ambazo zimewezesha kuanza kazi kwa karakana, kitengo cha uundaji, tanuru la uyeyushaji chuma na kitengo cha kuweka utando kwenye chuma ili kuzuia kutu.
Akizungumza leo Jumatano Machi 13, 2024 baada ya kutembelea kiwanda hicho, mwenyekiti wa kamati hiyo, Deodatus Mwanyika amesema kiwanda hicho ambacho ni cha muda mrefu, kilianzishwa kwa malengo makubwa lakini kwa bahati mbaya kilisimama kufanya kazi kwa muda mrefu.
Amesema kiwanda hicho ni muhimu katika kuzalisha viwanda vingine nchini, hivyo kinahitaji kutazamwa na kuongezewa nguvu ili kufikia malengo yaliyokuwa yamekusudiwa na Serikali wakati wa kuanzishwa kwake.
"Jitihada za kutafuta mwekezaji huko nyuma zilishindikana kwa sababu siyo rahisi ukapata mwekezaji akaja nchini kwako kutengeneza mashine za kusaidia watu wako kwani walio wengi wanataka kuuza mashine.
"Kwa hiyo, kiwanda hiki Serikali ina kila sababu ya kukiangalia kwa jicho la tofauti, tukienda kutafuta mwekezaji hapa tutakesha na unaweza ukapata ambao sidhani kama watakuwa na nia nzuri,"amesema Mwanyika.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema zaidi ya miaka 30 kiwanda hicho hakijafanya kazi na Serikali imedhamiria kufufua viwanda mbalimbali ambavyo vimekufa.
"Kwa sasa kiwanda hiki kinafanya kazi na tumeanza kuyeyusha chuma sisi wenyewe hapa, vijana wa Kitanzania wamerejeshewa ajira zao ambazo zilikuwa zimesimama kwa muda mrefu, tumerejesha ajira 150 za Watanzania ambazo zilifutika miaka 40 iliyopita na sasa mwendo unaendelea.
"Taifa letu litajengwa kwa uchumi imara wa viwanda na huwezi kuwa na uchumi imara wa viwanda kama huna viwanda vya msingi vinavyoitwa viwanda mama," amesema
Kiongozi idara ya uzalishaji KMTC, Joseph Mrina amewaomba wabunge kuendelea kukilinda kiwanda hicho kwa kuwa mbali na kutengeneza vyuma na mashine mbalimbali, kinatengeneza ajira mbalimbali na kuchochea ukuaji wa uchumi.
"Tunaomba mkilinde kiwanda hiki na mkiwekee msisitizo ili kiweze kusimama kufanya kazi kikamilifu, kwa kuwa kinachochea ukuaji wa uchumi nchin,” amesem