Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati ya Bunge yaipa maagizo 10 TRC

13382 TRC+PIC TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mitaji na Uwekezaji (Pic), imetoa maagizo 10 kwa Shirika la Reli (TRC), yakiwamo kuwasilisha mkakati wa kupunguza gharama za uendeshaji na utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa (SGR).

Mwenyekiti wa kikao kilichofanyika juzi, Janet Mbene aliagiza majibu ya maagizo hayo yawasilishwe kwa kamati ifikapo Novemba.

Alisema kamati imeiagiza TRC kuwasilisha mkakati wa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kupunguza matumizi ambayo yamebainika kuwa makubwa.

“Kwa mfano, gharama za mishahara ni asilimia 17, gharama za uendeshaji ni asilimia 41, gharama za uchakavu ni asilimia 33. Gharama hizi ni kubwa, ili ufanisi uwe mkubwa gharama za uendeshaji hazipaswi kuwa kubwa mno,” alisema.

Mbene ambaye ni mbunge wa Ileje alisema mkakati unaotakiwa kuwasilishwa na TRC ni wa jinsi wanavyoweza kuuza vyuma chakavu vinavyotokana na miundombinu iliyochakaa.

Alisema wakiuza wanaweza kupata hata Sh51 bilioni zinazoweza kutumika kuboreshea huduma.

Mwenyekiti huyo alisema TRC inaweza kuongeza safari za treni kama ilivyo jijini Dar es Salaam kwa kuwa ni miongoni mwa njia zinazoweza kuwaingizia fedha nyingi.

Kuhusu usafirishaji wa mizigo, alisema kwa mwaka wa fedha wa 2016/17, shirika hilo lililenga kukusanya Sh41 bilioni, lakini lilikusanya Sh19.6 bilioni (sawa na asilimia 47).

Mbene alisema katika usafirishaji wa abiria, TRC ililenga kukusanya Sh16.1 bilioni, lakini ilikusanya Sh12.2 bilioni (sawa na asilimia 76).

Alisema katika usafirishaji wa abiria ndani ya jijini la Dar es Salaam, shirika hilo lililenga kupata Sh539 milioni, lakini lilikusanya Sh2.2 bilioni.

Mbene alisema TRC ililenga kukusanya Sh58.5 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2016/17, lakini ilikusanya Sh34.1 bilioni (sawa na asilimia 58) ya malengo.

Alisema hilo lilitokana na uchakavu wa miundombinu na matatizo mengine.

“Tumegundua hawana sera ya uwekezaji, tumewaagiza watuletee sera yao ambayo itatuonyesha wanaenda kuwekeza wapi. Pia, tumewaambia watuletee mkakati wa kuboresha reli tuliyonayo wakati wakisubiri (reli ya kisasa) SGR.”

Mbene alisema shirika hilo linaruhusiwa kukopa na kuingia ubia (PPP), hivyo wameagiza wapatiwe mkakati wa jinsi litakavyohakikisha SGR inafika Kigoma na Mwanza badala ya kutegemea Serikali Kuu.

Mwenyekiti huyo alisema kuna fedha zinazotokana na uagizaji wa bidhaa nje ambazo zimetengenezewa mfuko lengo likiwa ni kugharamia utengenezaji wa miundombinu ya reli.

“Inaonekana fedha hizi ni kama Serikali inataka zote ziende kwenye SGR, sisi tunataka waje na mpango kiasi gani zinaenda katika reli iliyopo sasa. Hizi fedha zote ziko Benki Kuu, je wanapotaka kuzitumia wanazipata kwa urahisi au ikoje,” alisema.

Mbene alisema wameagiza kupelekewa mikakati ya kuhakikisha ufanisi wa shirika hilo haupungui wakati wa ukarabati wa madaraja, kuongeza vipande vya reli uzito na kurejesha vipande ambavyo viliondolewa katika mradi unaogharimiwa na fedha kutoka Benki ya Dunia wa Dola300 za Marekani (zaidi ya Sh675 bilioni).

Agizo lingine la kamati ni shirika hilo kuwasilisha mkakati wa kumaliza tatizo la kuharibika kipande cha reli kati ya Gulwe na Kilosa ambalo limekuwa likijitokeza kila mwaka kipindi cha mvua.

“Watu wamekuwa wakikwamia hapo na kuchukuliwa na mabasi. Sasa hii ni kero ya miaka mingi ambayo tumeona inaweza kumalizwa kwa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu,” alisema.

Pia wameagiza kupatiwa mkakati wa uandaaji wa umeme utakaotumika kwenye reli ya kisasa, rasilimali watu, ulinzi na vitu vyote vitakavyoendana na uendeshaji wake.

TRC inatakiwa kupeleka mbele ya kamati orodha na mkakati wa kulipa madeni yakiwamo waliyoyaridhi kutoka mashirika ya TRL na Rahco ambayo yaliunganishwa.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya TRC, Profesa John Kondoro alisema bodi ya shirika hilo iliundwa mwezi Machi, hivyo baadhi ya sera hazipo.

“Kuna vitu havikuwa wazi kwa sababu ni miradi inayoendelea. Kwa mfano, SGR tayari kuna mazungumzo na mradi ulianza mapema chini ya Rahco. Lakini mmezungumza mambo ya upatikanaji wa umeme na mengine ambayo yapo katika mpango,” alisema Profesa Kondoro.

Alisema kwa sababu ya muda hawakuweza kueleza kwa kina kuhusu mradi wa reli ya kisasa kwa kamati hiyo, hivyo wameahidi kurudi kuuelezea.

Chanzo: mwananchi.co.tz