Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati ya Bajeti yabadili msimamo ETS

63249 Kamatipic

Tue, 18 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Bajeti imeunga mkono mkakati wa Serikali wa kuongeza mapato kwa kutumia risiti za kielektroniki (ETS) na kusema utasaidia kukusanya mapato.

Kuungwa mkono huko kumekuja wakati taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zikionyesha ongezeko la ushuru wa forodha kutokana na bidhaa zinazotozwa kupitia stempu za kielektroniki.

Taasisi ya Uswisi, Société Industrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (Sicpa) ndiyo iliyoshinda tenda ya kuendesha mtandao na miundombinu ya mfumo wa ETS.

Awamu ya kwanza ya programu ya ETS ilifanywa Januari 15, 2019, ambapo stempu za kielektroniki ziliwekwa katika kampuni 19 zinazozalisha vileo, mvinyo na pombe kali.

Awamu ya pili ambayo itakwenda na uwekaji wa stempu kwenye viwanda vinavyozalisha vinywaji vyenye carbon na maji ya chupa ulitarajiwa kuanza Juni, mwaka huu.

Taarifa za TRA zinaonyesha kuwa baada ya kuanza kuweka stempu za kielektroniki, ushuru wa forodha ulipanda kutoka Sh24 bilioni Januari hadi Sh28 bilioni Aprili.

Pia Soma

Akichangia mjadala wa bajeti ya Sh33.1 trilioni jana, mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, George Simbachawene (Kibakwe-CCM), alisema kwa ujumla kamati yake imeridhishwa na ongezeko la kodi kutokana na matumizi ya stempu za kielektroniki kwa mwaka 2018/19.

“Kamati imefurahia ongezeko la mapato kupitia ETS na Serikali imekuwa ikizifanyia kazi changamoto za mfumo uliopo,” alisema.

Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango alitangaza mfumo wa ETS wakati akiwasilisha Bajeti ya mwaka 2018/19 Juni mwaka jana, akisema utawezesha Serikali kuwa na teknolojia ya kisasa ya kutoa taarifa kwa wakati kutoka kwa wazalishaji.

Alisema mfumo huo ulilenga kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuwezesha kujua mapato yatakayopatikana kupitia ushuru wa forodha, kodi ya ongezeko la thamani (Vat) na kodi ya mapato.

Hata hivyo, ETS ilikumbana na pingamizi kutoka Kamati ya Bajeti wakati huo, ikiongozwa na Hawa Ghasia na wabunge wengine wakidai kuwa mfumo huo ungeongeza gharama za uzalishaji wa bidhaa kama vile maji, sigara, vinywaji baridi, pombe kali na bia.

Kwa ujumla, Kamati ya Bunge ya Bajeti iliunga mkono uamuzi wa Serikali kufanya marekebisho ya vifungu 17 katika mwaka 21018/19 vilivyowezesha ongezeko la ukusanyaji wa mapato.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz