MKUU wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego ameunda kamati itakayoanza leo kushughulikia changamoto mbalimbali za machinga.
Hatua hiyo inayolenga kuyapa nguvu makubaliano yanayowataka wafanyabiashara hao wadogo wa mjini Iringa kurejea katika soko lao la Mlandege.
Kamati hiyo inayojumuisha idara mbalimbali za serikali inahusisha wawakilishi 24 wa machinga hao zaidi ya 700 wanaojihusha na biashara ya mitumba, malimbichi, upishi na maduka madogo.
Imeundwa baada ya jana jioni Mkuu wa Mkoa kukutana na machinga hao walioitikia wito wake wa kurejea katika soko hilo baada ya hivi karibuni kutangaza kurudi katika maeneo yao ya awali yasio rasmi katikati ya mji wa Iringa kwa kile walichodai serikali inachelewa kuyafanyia kazi madai yao mbalimbali.
Katika kikao hicho cha jana, machinga hao waliosema wamechoka kufanya migomo, maandamano na vurugu, waliwasilisha maombi yao mbalimbali kwa Mkuu wa Mkoa na kuahidi kama yakifanyiwa kazi hawatatoka tena katika soko hilo la Mlandege.
Maombi yao hayo ni pamoja na soko hilo la Mlandege ndio liwe soko la jumla la malimbichi zote kama ndizi, nyanya, viazi njegele na zinginezo zinazoingia katika masoko mbalimbali ya mjini Iringa.
Mengine ni kuwarudisha katika soko hilo machinga wote waliobaki katika maeneo yasio rasmi vikiwemo vichochoro vya mjini Iringa, huduma ya usafiri wa bajaji na daladala ipite katika soko hilo, huduma ya maji itawanywe, kuwe na mnada mmoja wa kila wiki, vifaa vya kukusanya taka na wakopeshwe mitaji.
Ombi lao lingine katika soko hilo lililojengwa kwa ufadhili wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Salim Asas ni pamoja na kupunguza gharama ya huduma ya choo kutoka Sh 200 hadi Sh 50 na kujenga choo kingine ili kusogeza jirani zaidi huduma hiyo karibu na watu wao.
Akiunda kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi maombi hayo, Dendego aliwataka machinga hao wasibebe ajenda za watu wanapotaka changamoto zao zishughulikiwe na akawataka wajiepushe na mashinikizo ya kufanya migomo wanayopewa na watu hao akisema kama wana jambo watumie ofisi za serikali kufikisha ujumbe wao.
“Na ili mawasiliano na viongozi wa serikali yawe rahisi, serikali inatoa ofisi ya muda katika soko la Mwamwindi mtakayoitumia kupokea na kushughulikia changamoto zenu mbalimbali kabla ya kufikishwa serikali,” alisema na kuongeza kwamba mkoa umekwishapokea Sh Milioni 10 zilizotolewa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa ofisi rasmi ya machinga.
Aidha Mkuu wa Mkoa alizungumzia suala la uongozi wa machinga mkoani Iringa akisema ni lazima mgawanyo wake ueleweke vyema.
“Tunataka kuona kila soko la machinga linakuwa na viongozi wake tofauti na viongozi wa wilaya na mkoa ili kurahisisha mawasiliano na kuondoa tofauti za kiutendaji,” alisema.
Aliyasema hayo baada ya hoja ya kujiuzulu kwa viongozi wa machinga wa Iringa, Yahaya Mpelembwa na katibu wake Joseph Mwanakijiji kuibuka katika kikao hicho ikilenga warudishwe katika nafasi zao na yeye kuzuia mjadala huo akisema suala hilo lishughulikiwe kwa kuzingatia katiba ya machinga na kwamba waliojizulu walikuwa na haki ya kufanya hivyo.