Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati Bunge yaibua kashfa stempu za TRA

Thu, 21 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wakati Kamati ya Bunge ya Bajeti ikiibua kashfa katika Stempu za Kielektroniki (ETS), wabunge wameitaka Serikali kusitisha mkataba na kampuni inayotekeleza mradi huo.

Wabunge pia wametaka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) lipewe kazi ya kuutekeleza mradi huo wa kuweka stempu za kodi kwenye bidhaa.

Mpango huo umekuwa ukipingwa na wafanyabiashara na Chama cha Wamiliki wa Viwanda (CTI) kwa madai kuwa utaongeza gharama za uzalishaji na kufanya bidhaa za hapa nchini kutoweza kushindana na za nje.

CTI na wafanyabiashara wanataka gharama za uwekezaji wa mradi huo zibebwe na Serikali badala ya wafanyabiashara kwa kuwa ndiyo inayonufaika kwa kudhibiti makusanyo.

SICPA (Societe Industrielle de Produits Alimentaire) ya Uswisi itawekeza Sh48 bilioni katika mradi huo wa kuweka kifaa cha kupiga stempu kiwandani kwa ajili ya kudhibiti bidhaa na kurahisisha ukusanyaji kodi, lakini itakuwa ikivuna Sh66 bilioni kila mwaka, kwa mujibu wa wabunge.

“Nilitaka kujiridhisha (kama) Serikali imejiridhisha na huyu aliyepewa kazi hii,” alisema mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu ambaye ni mmoja wa wenyeviti watatu wa Bunge.

“Ukitazama taarifa (za SICPA), ana matatizo makubwa. Ana kesi Morocco wamefanya ‘price offering’ (wametoa bei) mara kumi zaidi ya nchi nyingine walizofanya kazi hii.”

Zungu alisema kampuni hiyo inachunguzwa na bunge la Kenya na imeziangusha Serikali nyingine kutokana na mfumo wake wa rushwa.

“Tulifanya semina ya (Mamlaka ya Mapato Tanzania) TRA na wabunge, hoja zilizoulizwa kwenye semina walishindwa kuzijibu kutokana na kuwa za msingi na za kizalendo,” alisema Zungu.

“Kwa gharama (uwekezaji) za mradi huu za Sh48 bilioni, ibadilishwe mpango wa kuajiri watu wa nje kusimamia makusanyo ya kodi nchini.”

Aliiomba Serikali shughuli za mradi huo zifanywe na TTCL ambayo ina uwezo na ni chombo cha umma.

Sakata la kashfa ya mradi huo lilianza juzi wakati mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia alipokuwa akisoma maoni ya kamati bungeni.

Ghasia alisema mfumo wa kampuni hiyo unamtaka mwekezaji kurudisha gharama zake za uwekezaji kwa kutoza stampu ya kielektroniki kwa kila bidhaa itakayozalishwa.

Kiasi cha fedha kinachotarajiwa kuwekezwa na SICPA alisema ni dola 21.5 za Kimarekani (sawa na Sh48.5 bilioni).

“Kamati haina pingamizi na uanzishwaji wa mfumo huu, jambo la msingi ambalo linahitaji lifanyike kwa umakini ni kujiridhisha na gharama za mfumo huo ambazo zitabebwa na watumiaji wa bidhaa na mapato atakayoyapata mwekezaji kutokana na stempu,” alisema Ghasia.

Alisema kamati inashauri kuwa hatua ya Serikali kutoongeza ushuru wa bidhaa zisizo za petroli itakuwa haina maana kama gharama ya stempu itabaki kama ilivyopangwa.

Ghasia, ambaye ni mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), alisema hatua hiyo itasababisha kuongezeka kwa bei kwenye vinywaji kama vile maji, soda, bia na juisi ambazo sasa hazitozwi ushuru wa stempu.

Alisema kamati imefanya uchambuzi ili kubaini kiwango cha fedha ambacho kampuni ya SICPA itakipata katika mkataba huo kwa mwaka mmoja.

Alisema uchambuzi huo umehusisha takwimu za bidhaa tatu za maji, soda na sigara bila spiriti kwa kuangalia viwango vya uzalishaji wa bidhaa hizo kwa mwaka.

Alisema kiwango kinachozalishwa nchini kwa mwaka ni, maji lita 268,702,209 za ujazo, soda (lita 732,315,008), bia (lita 409,274,746) na sigara pakiti 429,310,400.

“Ukikadiria kwamba stempu itatozwa kwa idadi (unit) na si kwa ujazo (lita), chupa moja ya bia ya mililita 500 itatozwa Sh22.73, soda ya ujazo huo (Sh13.5), spiriti mililita 1,000 itatozwa Sh29.57,” alisema Ghasia.

Alisema mzigo huo utabebwa na mlaji wa mwisho.

“Kwa mantiki hii, ukokotoaji unaonyesha kwa mwaka mmoja SICPA itakusanya jumla ya Sh66.7 bilioni bila kuhusisha takwimu za bidhaa ya spiriti. Kiasi hiki ni kikubwa kuliko alichowekeza katika kipindi cha mwaka mmoja tu wa mkataba,” alisema Ghasia.

Alishauri Serikali kuwekeza katika mradi huo kwa Sh48.5 bilioni ili makusanyo yawe sehemu ya mapato yake badala ya kuchukuliwa na kampuni binafsi.

Ingawa katika baadhi ya nchi imeibuka kidedea, SICPA imekuwa na matatizo katika nchi mbalimbali ambazo iliingia nazo mkataba wa kuweka stempu kwenye bidhaa.

Chanzo: mwananchi.co.tz