Mkuranga. Licha ya kuwa na miundombinu yote ya umeme, wakazi wa vijiji 17 kutoka kata tatu za wilaya ya Mkuranga hawana huduma hiyo hali inayosababisha kushindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
Miundombinu hiyo imewekwa tangu 2014 lakini mpaka sasa wakazi hao hawajapata umeme.
Hata hivyo, wanaweza wakaondokana na changamoto ndani ya siku 14 baada ya Serikali kuwaahidi kulishughulikia tatizo hilo.
Wakizungumza na mbele ya Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani leo Agosti 7, 2018 wamesema kukosekana kwa umeme kunawakosesha vijana wa eneo hilo ajira.
"Hapa kuna viwanda vinne kikiwamo cha kusindika dagaa kamba na kutengeneza boti za kisasa ambavyo vyote vimefungwa," amesema Ramadhan Hamis mkazi wa eneo hilo.
Naye Maulid Mwinyimkuu, amesema wanapata kero kwa kukosekana umeme na hatua inayosababisha kufuata huduma muhimu Mkuranga mjini.
"Hadi kuchaji simu tunakwenda mjini kufuata huduma hii, hali yetu ni mbaya na tunakosa maendeleo kwa kukosa nishati hii. Tulikubali minazi yetu na miembe ikatwe ili kupisha Rea lakini hatuoni matunda yake," amesema.
Akizungumzia changamoto hiyo, Dk Kalemani ameanza kwa kusema: " Hii haingii akilini yaani nguzo zipo, lakini umeme hakuna. Nawaomba watendaji wa Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania ) waje mbele yenu.”
Baada ya kuwaita watendaji hao, Dk Kalemani amesema makosa yalifanyika kwa Tanesco kumuachia mkandarasi MBH aliyekuwa akitekeleza awamu ya pili ya Rea bila kukamilisha kazi hiyo.
"Mmewaona hawa watendaji? Hawa ndiyo watakaosimamia mradi huu kwa sawa hadi ukamilike nawapa siku 14. Kuanzia kesho (leo) nataka kazi ianze,” ameagiza.
Aliwataka watendaji kutafuta mafundi popote walipo kwa ajili ya kuanza kazi ili wakazi wa vijiji hivyo wapate nishati hiyo walioikosa kwa muda mrefu.