Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amesema alitarajia Rais John Magufuli kumuondoa katika wizara hiyo.
Amesema alilitarajia hilo kutokana na mazingira yaliyokuwa jana Ijumaa Juni 7, 2019 katika mkutano kati ya Rais John Magufuli na wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka Wilaya zote nchini Tanzania uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Leo Jumamosi Juni 8, 2019 Rais Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri kwa kutengua uteuzi wa Kakunda na kumteua aliyekuwa naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
Kakunda ambaye leo Jumamosi Juni 8, 2019 ametimiza siku 210 tangu alipoteuliwa kuongoza Wizara hiyo akichukua nafasi ya Charles Mwijage ambaye pia aliondolewa, amesema kwa jinsi wafanyabiashara walivyotoa malalamiko yao Ikulu na kuinyooshea kidole Wizara ya Viwanda wakidai haiwatendei haki, kama kiongozi ilipaswa kujiuzulu.
Miongoni mwa kero zilizotajwa na wafanyabiashara hao ni utitiri wa kodi, vibali vya kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi, urasimu katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na madai ya watendaji wa wizara ya Viwanda na Biashara kujisifu kuvifunga viwanda kutokana na dosari mbalimbali na madai ya kodi na ushuru.
Kuhusu mafanikio yake katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Kakunda amesema hawezi kujisifu kwa chochote kwa sababu kazi aliyoifanya ilikuwa ni ya Serikali na aliifanya kama timu pamoja na wasaidizi wake.
Habari zinazohusiana na hii
- Magufuli: Nimefuta tozo 101 tangu nilipoingia madarakani
- VIDEO: Rais Magufuli atamani kuona mabilionea wengi Tanzania
- VIDEO: Mambo matano yaliyoibua mjadala Rais Magufuli akikutana na wafanyabiashara
- Rais wa Tanzania aeleza wafanyabiashara wanavyokwepa kodi