Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kakoko: Bandari ya Bagamoyo ingefilisi Serikali

58773 Bandari+pic

Tue, 21 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Serikali imedai masharti magumu yaliyotolewa na mwekezaji ndiyo sababu ya kusitisha majadiliano kuhusu mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Masharti hayo ni pamoja na mwekezaji kupewa uhuru wa kujipangia bei ya kutoza wanaosafirisha mizigo kupitia bandari hiyo, kusamehewa kodi na ushuru mbalimbali zikiwemo zile za lazima kisheria pamoja na kulipwa fidia ya hasara ya kibiashara katika hesabu watakazopitia wao wenyewe.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Mwanza juzi, mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedith Kakoko alisema si tu baadhi ya masharti hayo yangefilisi Serikali, bali yangesababisha nchi na watu wake kuuzwa.

“Pamoja na kujipangia bei, pia (wawekezaji) walitaka kusamehewa kodi zote kwa madai kuwa hakuna shehena ya kutosha; hakuna shehena ya kutosha wakati wewe (mwekezaji) unataka kuwekeza kwenye reli na bandari. Unakuja kwa sababu biashara ipo” alisema na kuhoji Kakoko.

“Kibaya zaidi, wakaja na sharti kuwa wakipata hasara kwa mujibu wa mahesabu yao wenyewe ambayo hatujui watayafanyaje, Serikali iwafidie. Nani anajua watapata hasara. Hii inaweza kuifilisi Serikali na nchi ikauzwa hata na wananchi wake,” aliongeza.

Alisema wakati wawekezaji wakidai hakuna shehena ya kutosha, utafiti na uchunguzi wa kina wa Serikali umebaini walipanga kumiliki biashara ya bandari na usafirishaji kwa njia ya reli kurahisisha usafirishaji wa shenena ya shaba kutoka nchi za Zambia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Pia Soma

“Walichotaka kufanya baada ya kuchukua mifumo ya usafirishaji (reli) na bandari ni kusafirisha shehena za shaba kutoka Zambia na DRC lakini kodi, mahesabu yote na ukaguzi unafanyika China,” alisema Kakoko.

“Sisi tungeaminishwa mizigo yote imesafirishwa bure na wao kwenda kulipana huko kwao na ingekuwa rahisi kwa sababu mwenye shehena ni mwekezaji, anayesafirisha ni mwekezaji na mwenye bandari ni mwekezaji huyo huyo,” alisema.

Kuhusu vivutio kwa mwekezaji, Kakoko alisema Serikali ilikuwa tayari kusamehe baadhi ya tozo ikiwemo ushuru wa stempu, ukaguzi wa forodha (customs inspection) ile ya ukaguzi wa meli ambayo ni ya kimataifa na huwa haiondolewi.

Alisema Serikali pia ilikuwa imekubali kuanzisha kituo kimoja (one stop center) maalumu kwa ajili ya kuhudumia biashara katika Bandari ya Bagamoyo.

“Lakini ajabu wenzetu wakaja na masharti mengine mapya karibia 14 ikiwemo kusamehemewa kodi ya mapato, kodi ya taasisi, kodi ya ongezeko la thamani ya mali, kodi ya mapato kwa watu binafsi, ushuru wa Serikali za mitaa na kodi ya majengo,” alisema Kakoko.

Kodi nyingine ambazo mwekezaji alitoa masharti ya kuondolewa ni tozo ya ardhi, kodi ya fidia kwa wafanyakazi, kodi ya uendelezaji wa ujuzi, kodi ya forodha na kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT.

Kwa mujibu wa Kakoko, mwekezaji pia aliweka sharti la kuondolewa kwa kodi, ushuru na tozo zote za vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini, sharti alilosema lingesababisha wageni, hata wasiohitajika wala kuwa na kazi ya kufanya kujazana nchini.

“Hata kama ingebidi kuwaachia (kuwasamehe kodi) inabidi tuangalie ni kwa asilimia ngapi. Lakini wao walitaka (wawekeze) bure kabisa, hii ni kuuza uhuru wa nchi,” alisema.

Alisema Serikali haijafunga milango ya majadiliano, lakini akasisitiza kuwa maslahi ya Taifa yatakuwa mbele ya kila kitu katika majadiliano, utekelezaji na uendeshaji wa miradi yote ya uwekezaji.

“Tunawasubiri. Wakilegeza masharti na kukubali tugawane sawa sawa hakuna tatizo; waje tu na fedha zao. Lakini wahakikishe nasi tunapata. Wakitaka wao wapate asilimia 100 na sisi tuambulie sifuri….mie nadhani kila mwenye akili timamu ataelewa hiyo,” alisema Kakoko.

Huku akisisitiza umuhimu na faida ya kujengwa kwa Bandari ya Bagamoyo, Kakoko alisema bila kujali mwekezaji anatoka nchi gani, Serikali itahakikisha kila upande unanufaika.

“Tuna mtaji wa ardhi na rasilimali watu na mwekezaji ana mtaji, lazima pawepo pata nipate,” alisisitiza.

Chanzo: mwananchi.co.tz