Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kairuki ataka miundombinu kwa wawekezaji

56952 Pic+kairuki Kairuki ataka miundombinu kwa wawekezaji

Wed, 1 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki, ameiomba mikoa na halmashauri kutenga maeneo ya uwekezaji na kuyawekea miundombinu stahiki ili kuwavutia wawekezaji.

Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku 5 katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya iliyomsaidia kujifunza, kujionea uwekezaji pamoja na kuzungumza na wawekezaji katika ukanda huo.

Alikipongeza Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), kwa kuwa mfano mzuri katika kuhamasisha uwekezaji, na kutaka taasisi zingine kuiga mfano huo.

Waziri alisema mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwamo za utalii, kilimo na ufugaji.

Aliwahimiza wakuu wa mikoa na halmashauri kutenga maeneo ya uwekezaji na kuyawekea miundombinu stahiki ili kuendelea kuvutia wawekezaji nchini.

“Kila mkoa na halmashauri zake ni vizuri kutenga maeneo ya uwekezaji sambamba na kuweka miundombinu rafiki ili kuwatia moyo wawekezaji wa nje na ndani kuwekeza nchini,” alisema Waziri Kairuki.

Alisema serikali inaweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kuwavutia wawekezaji kufanya shughuli na kukuza la pato taifa.

Aliwataka wawekezaji kujisajili kwa hiari kwenye Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) ili kunufaika na fursa zilizomo katika kituo hicho.

Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Geoffrey Kirenga, alisema kituo kitaunganisha nguvu kutoka sekta za umma na binafsi ili kutoa mchango chanya katika maendeleo ya taifa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live