Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kairuki ahamasisha uwekezaji kwenye mkonge

10562 Pic+kairuki Kairuki ahamasisha uwekezaji kwenye mkonge

Mon, 6 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Angela Kairuki, amewataka wananchi kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri za wilaya, kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kuwekeza katika kilimo cha mkonge, ambao imeonekana kuwa na chachu kubwa ya maendeleo.

Kairuki, alitoa rai hiyo jana, baada ya kutembelea shamba la mkonge la Kisangara, lililoko chini ya Kampuni ya Mohamed Enterprises, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro na kupewa taarifa ya upungufu wa mashine kwa ajili ya kuchakata zao hilo.

Waziri Kairuki alisema ni fursa kubwa kwa wananchi kujipatia kipato na wanaweza wakajiunga katika vikundi kama na kupewa mkopo, ambao watauwekeza katika ununuzi wa mashine ya kuchakatia mkonge, ijulikanayo kwa jina maarufu kama ‘Corona’ na kupiga hatua kimaendeleo.

“Nimeelezwa kuwa, kuna upungufu wa mashine za kuchakata mkonge, hivyo wakati mwingine mkonge upo ila hakuna mashine ya kuchakata, sasa viongozi wa halmashauri na hata mkoa, tuendelee kuwahamasisha wananchi wawekeze katika zao la mkonge, ambako kumeonekana kuwa na fursa nzuri,” alisema Kairuki na kuongeza:

“Tunaweza pia kutumia fursa ya mikopo ya wanawake, kikundi au vikundi vya ushirika vinaweza kuwekeza katika Corona wananchi wachangamkie fursa hii, ili kumaliza tatizo la upungufu wa mashine hizi.”

Aliwataka viongozi wa halmashauri, kutoa elimu kwa wananchi na kuelezea fursa zilizopo katika mkonge, ili kupanua wigo wa uwekezaji katika kilimo hicho, kwa kuwa mahitaji ya mkonge bado ni makubwa nchini na hata duniani.

“Mahitaji ya mkonge bado ni makubwa, hivyo tuendelee kuhamasisha wananchi na kuwapa elimu ili wale wenye maeneo yanayofaa kwa kilimo hicho, waweze kuwekeza huko, lakini pia tunaendelea kukaribisha wawekezaji wengine, kuingia katika uchakataji wa zao hili, kwa kuwa kwa sasa vipo viwanda zaidi ya 11 vikubwa na vya kati vya kuchakata mkonge, na viwanda vidogo zaidi ya 70 kwa ajili ya uchakataji wa zao hili,” alisema.

Awali, akizungumza Meneja wa kituo cha uwekezaji Kanda ya Kaskazini, Daudi Riganda, aliutaka uongozi wa shamba hilo, kuongeza uzalishaji na kuwekeza zaidi katika zao hilo ili kutengeneza faida.

“Bado hatujaridhika na mwekezaji ametumia fursa ya uwekezaji katika kilimo hiki cha mkonge, ikilinganishwa na rasilimali ya ardhi aliyo nayo na hali ya hali ya hewa iliyopo, hivyo ningeshauri, wawekezaji watakaopewa nafasi ya kuwekeza katika kilimo cha mkonge, waongeze uzalishaji na kuwekeza kwa tija zaidi,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson, alisema kwa sasa wanajipanga kutoa elimu na kuhamasisha wananchi, kujiingiza katika kilimo cha mkonge, ili kuboresha maisha yao kwa kutumia fursa zilizopo nchini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live