Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kairuki: Tutafanya mapinduzi ya uhifadhi wanyamapori

Anjella Kairuki SS Kairuki: Tutafanya mapinduzi ya uhifadhi wanyamapori

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Angellah Kairuki amesema Serikali imechukua hatua madhubuti za kuboresha utendaji kazi na kuleta mapinduzi katika utoaji huduma na utatuzi wa changamoto katika sekta ya uhifadhi wa wanyamapori.

Akizungumza mjini Babati mkoani Manyara wakati wa maadhimisho ya siku ya wanyamapori duniani leo Jumatatu Machi 4, 2024, Waziri Kairuki amefafanua kuwa Serikali inalenga kujikita katika matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na misitu.

Kairuki amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha uhifadhi unakuwa endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa mujibu wa Kairuki, Serikali imeandaa mikakati mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutekeleza sera ya wanyamapori wa mwaka 2023-2033, mkakati wa kitaifa wa kupambana na ujangili wa mwaka 2023-2033, na mpango mkakati wa kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu wa mwaka 2020-2024.

Kairuki alizungumzia pia hatua za kukabiliana na changamoto za sekta hiyo, kama vile ujangili, biashara haramu ya nyara na mazao ya misitu, uvamizi wa maeneo ya hifadhi, shoroba na mtawanyiko wa wanyamapor bila kusahau kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi.

Alifafanua kuwaS imejizatiti kutatua changamoto hizo kupitia mikakati iliyowekwa, na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano na wadau wa uhifadhi.

Aidha, Waziri Kairuki aligusia hatua za kimataifa zilizochukuliwa na Tanzania kwa kuridhia mkataba wa biashara ya wanyamapori na mimea iliyo hatarini kutoweka mwaka 1979 na kuimarisha usimamizi, ulinzi, na uhifadhi wa maliasili.

Alitaja pia ushirikiano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na wizara nyingine katika kuandaa na kusimamia mipango ya matumizi ya ardhi, ikiwa ni njia ya kupunguza uvamizi katika maeneo ya hifadhi na shoroba za wanyamapori.

Kairuki alisisitiza mbinu nyingine za kukabiliana na changamoto za uhifadhi wa wanyamapori, kama vile kuhamasisha jamii kuanzisha maeneo ya ufugaji wa wanyamapori na kuanzisha maeneo ya jumuiya za hifadhi za wanyamapori jamii (WMA).

Alimalizia kwa kutoa wito wa ushirikiano wa Serikali na wadau wengine katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kutoa mfano wa tamasha la utalii lililofanyika hivi karibuni wilayani Same, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha shughuli za utalii nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, aliwapongeza wanafunzi na wadau wa mazingira kwa kuchangia upandaji wa miti 2,000 katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Alisisitiza umuhimu wa kuyalinda mazingira kwa kurejesha uoto wa asili, huku akihamasisha juhudi za pamoja kwa ajili ya maendeleo endelevu na kudumisha mazingira bora.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live