Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kahawa ya Tanzania dili soko la kimataifa

76fde029248e681a9d8b76dbe3657f5c Kahawa ya Tanzania dili soko la kimataifa

Wed, 6 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BODI ya Kahawa Tanzania (TCB), imesema kuna soko la uhakika la kahawa ya Tanzania kwenye soko la dunia na kiasi kinachopelekwa huko hakikidhi mahitaji.

Mwenyekiti wa TCB, Profesa Aurelia Kamuzora, amesema kuna mahitaji makubwa ya kahawa ya Tanzania kwenye masoko ya kimataifa.

Alisema hayo mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kahawa Duniani.

"Soko la kahawa ya Tanzania lipo kubwa na mahitaji ya kahawa yetu tunayozalisha ni makubwa ila kahawa bora inayokidhi mahitaji ya soko la dunia ni chache. Ipo kampuni ilipata tenda ya kusambaza kahawa zaidi ya tani 700 kwa mwezi ila walichanganyikiwa watapata wapi kahawa hiyo," alisema.

Profesa Kamuzora alisema TCB kwa kushirikiana na wadau wameongeza jitihada za uzalishaji wa zao hilo ili kukidhi mahitaji ya soko la dunia.

"Soko la uhakika wa kahawa yetu lipo, naona kuna ongezeko la wadau kuingia katika sekta hii kuongeza mnyororo wa thamani wa kahawa hivyo tunapaswa kuongeza juhudi, pia wakulima walime kwa wingi ikiwamo mikoa mipya inayoanza kulima ifanye kwa haraka ili tutosheleze soko la nje," alisema.

Wakati akifunga maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai, alisema unywaji wa kahawa umeongezeka duniani na kwamba kwa siku zaidi ya vikombe bilioni tatu hunywewa.

"Unywaji wa kahawa unakuwa kwa kasi, hivyo tunaona ni namna gani ni fursa kubwa ya uchumi kwa nchi yetu na tumehakikishiwa soko lipo ila tu kuna upungufu wa kukidhi mahitaji, niombe bodi kwa kushirikiana na sekta binafsi waongeze juhudi katika kuhamasisha uzalishaji wa kahawa bora nchini," alisema Kagaigai.

Alisema kuna haja ya kufanyika jitihada kuhakikisha wazalishaji wa kahawa wanakuwa na uhakika wa bei ili kuwapa hamasa kutokana na kuyumba kwa bei ya zao hilo mara kwa mara katika soko la dunia.

Mratibu wa kilimo cha kahawa Wilaya ya Moshi, Vailet Kisanga, aliiomba serikali na TCB waone umuhimu wa kuongeza makundi ya wanawake na vijana katika uzalishaji wa zao hilo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz