Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kahawa, samaki vyaongoza mauzo soko la UIaya

054d0d7077ed71fe9b035ecdfecb9a1d Kahawa, samaki vyaongoza mauzo soko la UIaya

Thu, 31 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kahawa kutoka Tanzania imeongoza kuuzwa katika soko la Ulaya (EU) kwa mwaka jana na kuingizia nchi takribani Euro milioni 68.

Hata hivyo, zao hilo kama Tanzania ikijipanga vyema imeelezwa kwamba linaweza kuuzwa hadi kufikia Euro milioni 168.

Hayo yamebainishwa kwenye ripoti iliyozinduliwa jana inayoonesha mchango wa uwekezaji ya EU kwa Tanzania na namna umoja huo unavyochangia maendeleo ya viwanda na maendeleo kwa ujumla.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mazao yanayofuatia ni samaki wabichi na kokoa, mazao ambayo pia yameelezwa kwamba yana nafasi kubwa ya kuuzwa zaidi ya kiwango cha sasa Ulaya.

Mazao mengine yaliyofanya vizuri kwenye soko la Ulaya ni ufuta, mbogamboga zinazolimwa kitaalamu (unrooted cuttings), parachichi na korosho.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania imeuza bidhaa zenye thamani ya Euro milioni 456 Ulaya huku nchi za Ulaya zikiingiza nchini bidhaa zenye thamani ya Euro milioni 856 katika kipindi hichohicho.

Bidhaa kubwa kutoka EU inayoingia nchini ni dawa za binadamu. Nyingine ni matrekta, magari, dawa za kuua wadudu, ngano, vifaa vya maabara, vipuri vya magari na kadhalika.

Ripoti hiyo ilizinduliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akizungumza baada ya uzinduzi wa ripoti hiyo, Waziri Mulamula alibainisha kuwa mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Rais Samia Suluhu Hassan yamechagiza kuendelea kuwepo uwekezaji mkubwa wa kampuni za EU hapa nchini.

“Hii ripoti imetuonesha matokeo ya hatua nzuri ambazo tumekuwa tunazichukua kama nchi katika kuvutia uwekezaji na pia inatuonesha wapi hasa tunatakiwa kuongeza nguvu zaidi katika kuvutia uwekezaji,” alisema.

Alisema kampuni takribani 100 za Ulaya zimewekeza nchini na kusababisha ajira 151,000 na kwamba asilimia 98 ya walioajiriwa kwenye kampuni hizo ni Watanzania, asilimia 38 wakiwa wanawake.

Mkurugenzi Mtendaji wa European Union Business Group (EUBG), iliyoshiriki kuandaa ripoti hiyo, Cikay Richards alibainisha kuwa kampuni za EU zimekuwa wawekezaji wakubwa nchini hususani katika sekta za kilimo na utalii.

Balozi wa EU nchini, Manfredo Fanti alisema ripoti hiyo mbali na kuonesha namna kampuni za EU zilivyowekeza nchini pia inaonesha fursa nyingi zaidi za kibiashara zilizopo Tanzania na kwa kiasi gani kampuni za nje zinaweza kuja kuwekeza.

Alisema mbali na kufanya biashara, EU imekuwa pia ikisaidia kuwainua wajasiriamali nchini kupitia benki yake ya uwekezaji (European Investment Bank) inayokopesha benki za Tanzania ili nazo zifikishe mikopo kwa wajasiriamali wadogo.

Alisema katika kuhakikisha Tanzania inazidi kunufaika na biashara kwa nchi za EU, umoja huo umeondoa kodi kwa bidhaa kutoka Tanzania.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, David Kihenzile aliutaka EU kuongeza uwekezaji zaidi katika kilimo, mifugo na utalii.

Akitoa mfano, alisema kupitia sekta ya mifugo Tanzania inatakiwa iwe inauza Ulaya bidhaa zitokanazo na mifugo kama ngozi na nyama.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live