Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KONA YA MMACHINGA: Kitunguu saumu ‘chamtoa’ Halima kimaisha

85363 Pic+kitunguu KONA YA MMACHINGA: Kitunguu saumu ‘chamtoa’ Halima kimaisha

Sat, 23 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kitunguu saumu ni moja kati ya viungo vinavyotajwa kutibu magonjwa mengi endapo vikitumika ipasavyo. Hata hivyo, watu wamekuwa wakishindwa kukitumia kutokana na changamoto ya kutokuwa na muda wa kutosha.

Jambo hili huwafanya watu kutafuta urahisi kwao hasa kwa kutafuta vile ambavyo tayari vimeandaliwa ili kurahisisha kazi yao na kuharakisha katika kupika.

Halima Kabali ni mmoja kati ya watu waliotumia fursa ya watu kukosa muda wa kuandaa kuamua kuwarahisishia watumiaji wa vitunguu saumu kwa kuvimenya, kusaga na kuviweka katika vifungashio.

Akiwa ni mhitimu wa programu ya uuguzi aliamua kuingia katika ujasiriamali huo Juni mwaka huu huku akiwa na mtaji wa Sh70,000.

Alifanikiwa kununua vitunguu vya Sh50,000, vifungashio vya Sh15,000 pamoja na kutengeneza nembo ya bidhaa kwa Sh5000.

“Nilifanikiwa kupata kopo 30 za miligramu 250 ambapo kila moja niliuza kwa Sh4000 na kutengeneza Sh120,000,” anasema Halima ambaye aliamua kuendelea kuwekeza fedha hiyo huku akibainisha kuwa hadi sasa kwa mwezi huuza hadi kopo 600 huku wateja wake akiwapata kupitia mitandao ya kijamii.

“Mpaka sasa mtaji wangu umefikia Sh1.1 milioni na ninauza bidhaa ndani ya mkoa na katika maeneo tofauti na wakati mwingine natumia super market kuuza,” anasema Halima.

Pia, anasema licha ya kukutana na changamoto kubwa ikiwamo upatikanaji wa nembo ya ubora wa bidhaa ambayo mara nyingi sharti lake kubwa ni kuwa na jengo maalumu la kutengeneza bidhaa lililo nje ya mji lakini ana ndoto za kufika mbali.

“Nataka niwe na kiwanda changu kwa ajili ya kutengenezea vitunguu saumu, nizalishe kwa wingi na niuze kimataifa,” anasema Halima.

Chanzo: mwananchi.co.tz