Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KMKM kilivyonasa sukari ya magendo

11353 Sukari+pic KMKM kilivyonasa sukari ya magendo

Mon, 1 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KIKOSI Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) kimefanikiwa kukamata jumla ya viroba 45 vya sukari vilivyokuwa vikisafirishwa kwa njia ya magendo maeneo ya bahari ya Nyamanzi kuelekea Bagamoyo, Tanzania Bara.

Kamanda Mkuu wa Operesheni ya kikosi hicho, Luteni Kheir Ahmada, alisema askari wake walikuwa katika doria za kawaida na kufanikiwa kukamata sukari hiyo.

Alisema kikosi chake kilifanikiwa kuikamata mashua ambayo haikuwa na jina wala namba za usajili ikiwa na virobo hivyo ikielekea Bagamoyo.

"Mashua hiyo ilikuwa na mabaharia watatu na tuliikamata juzi majira ya saa tano asubuhi ikielekea Bagamoyo," alisema.

Kamanda huyo aliwataja watuhumiwa ni nahodha Takdir Abdallah, Sheha Miraji Makungu na Ibrahim Mzee Hassan, wakazi wa Bagamoyo.

Alisema watuhumiwa hao chombo chao pamoja na sukari hiyo vimekabidhiwa kwa Mamalaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar kwa hatua zaidi za kisheria.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja, Hamida Mussa, alisema serikali imejipanga kupambana na biashara za magendo ambapo zimekuwa zikiikosesha serikali mapato.

Alisema serikali itahakikisha inadhibiti bandari zote zisizokuwa rasmi ili kuhakikisha hazitumiwi na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Aidha, aliipongeza KMKM kwa juhudi zake za kulinda mali za nchi na kuitaka kuzidisha juhudi na kuwa makini pamoja na kushirikiana na taasisi nyingine ili kupambana na wenye lengo la kuikosesha serikali mapato na kuhujumu uchumi wa nchi.

Kufuatia kujitokeza kwa uhaba wa sukari Tanzania Bara, baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitumia mwanya huo kusafirisha sukari kimagendo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live