Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) umejipanga kupokea idadi kubwa ya wasafiri wakiwemo watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani wapatao milioni 1.2 baada ya kufanya maboresho ya miundombinu yake kwa lengo la kukabiliana na ongezeko hilo.
Kabla ya mlipuko wa ugonjwa wa uviko 19 uwanja huo ulikuwa ukipokea abiria wapatao 850,000 kwa mwaka ambapo wamesema idadi ya abiria itaongezeka kutoka idadi hiyo hadi kufikia milioni 1.2 kutokana na mwitikio mkubwa wa filamu ya Royal Tour Kimataifa.
Kufuatia ongezeko hilo ,Wadau wa sekta ya utalii nchini wamekutana na Menejimenti ya uwanja huo wa ndege kutathmini namna ya kukabiliana na wimbi hilo kubwa la wasafiri wanaotegemewa kuingia nchini kupitia uwanja huo mwakani.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KADCO, Christine Mwakatobe amesema ujio huo wa watalii ni kutokana na mwitikio wa uandaaji wa filamu hiyo ambapo mashirika ya ndege kutoka Mataifa mbalimbali yataongeza safari zake hapa nchini pamoja ujio wa mashirika mapya ya ndege likiwemo shirika la ndege la Eurowings Discover pamoja na Turkish Airlines.
"Tuko hapa leo na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii kwa lengo la kujitathmini na kuangalia namna ya kukabiliana na wimbi kubwa la watalii tunaowategemea kuja hapa nchini kupitia uwanja wetu wa KIA kutokana na mwitikio wa filamu ya Royal Tour duniani,"
"Kufikia mwakani tutakuwa na wageni 1.2 milioni ikiwa ni pamoja na ujio mpya wa ndege pamoja na mashirika kurejesha safari zake hapa nchini.
Advertisement "Tunaendelea kuboresha miundombinu iliyopo ili iweze kuendana na ongezeko la abiria ,sasahivi tupo kwenye hatua za utekelezaji wa mradi wa kuboresha na kupanua eneo la maegesho ya magari uwanjani pamoja na kuboresha huduma za zima moto kwa kununua magari mapya,"
"Kama tunavyojua msimu wa utalii (High Season) unaanza siku chache zijazo hivyo tunatarajia kupata ugeni mkubwa wa watalii hivyo tunaangalia namna tutakavyojipanga ,kuangalia changamoto mbalimbali zilizopo na namna ya kukabiliana nazo ili tuweze kutoa huduma bora ili kutengeneza taswira nzuri mbele ya dunia," alisema
Akizungumzia namna walivyojipanga kupokea watalii hao,Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi(TANAPA),Beatrice Kessy amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wadau wa utalii ndani na nje ya nchi ambapo amesema Shirika hilo limejipanga kuboresha miundombinu ya barabara ,malazi katika hifadhi za Taifa ili kuhakikisha watalii hao wanapata huduma bora.
"Tumejipanga na tuna maeneo takribani 100 ya uwekezaji katika hifadhi zetu za Taifa na tunaendelea kutoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kutembelea maeneo ya uwekezajin ambayo yako katika hifadhi za Taifa ili wawekeze,"
"Tanapa tumekuwa na jitihada za kuweza na kuendeleza maeneo ya malazi ya gharama nafuu na kwasasa tuna miradi mbalimbali ya ujenzi wa hosteli ,maeneo ya kambi za kulaza wageni,kwa hiyo tumejipanga vyema kuhakikisha wageni wetu wanapata maeneo mazuri ya kulala,"alisema
Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai ,Juma Irando amesema ongezeko hilo la watalii litakuwa na faida kubwa kwa wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla kwani kutaongeza mapato ya nchi pamoja na mwananchi mmoja mmoja pamoja na kutoa ajira kwa vijana.
"Najua KIA ndio lango kuu la kuingiza watalii natarajia mtahakikisha mnaboresha huduma kwa kuzingatia viwango vilivyopo vya Kitaifa na Kimataifa ili kuvutia uwekezaji na mashirika mengi ya ndege ya Kimataifa,"alisema DC Irando.