Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KIA wapewa maagizo kuongeza idadi ya mashirika

Kilimanjaro Airport Terminal Building KIA wapewa maagizo kuongeza idadi ya mashirika

Thu, 19 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David kihenzile ameutaka uongozi wa Kampuni ya Uendeshwaji na Uendelezwaji wa kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro (Kadco) ambao ndiyo waendeshaji wa kiwanja cha ndege Kilimanjaro (KIA) kuongeza idadi ya mashirika yanayohudumia kutoka 13 yaliyopo sasa.

Kihenzile ameyasema hayo leo Oktoba 18, 2023 wakati akizungumza jijini Arusha wakati wa muendelezo wa ziara zake za kuongea na viongozi na kukagua miradi mbalimbali ambapo amewataka kuongeza ubunifu kwakuwa mashirika hayo ni machache ikilinganishwa na uwekezaji uliofanyika.

"Rais Samia Suluhu Hassan ameshaanza yeye mwenyewe kuigiza kwenye filamu ya Royal Tour ambapo alitua hapa ili kuvutia wageni zaidi sasa ni wakati wa kampuni kuwa na mikakati ya masoko inayoonekana, inayokubalika na inayotekelezeka ya kutafuta masoko nje ya nchi ili kuvutia mashirika ya kimataifa zaidi" amesema Kihenzile

Aidha, Kihenzile amesema yapo maagizo mengi hutolewa na viongozi mbalimbali ila utaratibu uliopo hakuna ufuatiliaji makini wa maagizo hayo hivyo ameielekeza Kampuni ya Uendeshwaji na Uendelezwaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Arusha kuhakikisha inawasilisha wizarani taarifa kamili ya maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi mbalimbali wa serikali kwa nyakati tofauti na utekelezaji wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kadco, Christine Mwakatobe amesema hali ya utendaji na shughuli mbalimbali za KIA kuanzia mwaka 2019 hadi 2023 ni wa ufanisi mkubwa ambapo idadi ya abiria imeongezeka kutoka abiria 794,337 mpaka 929,553, mizigo kutoka kilo milioni tatu mpaka milioni 4.3, idadi ya miruko kutoka 20,756 mpaka 22,715 huku mapato yakipanda kutoka Sh26 bilioni mwaka 2019/2020 mpaka Sh31.7 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 59.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live