KFC imetangaza kufunga migahawa yake yote nchini Lesotho kutokana na mlipuko mkali wa homa ya ndege katika nchi jirani ya Afrika Kusini.
Serikali ya Lesotho imepiga marufuku uagizaji wa kuku wote kutoka nchini humo, ambao KFC inasema "umeathiri pakubwa" usambazaji wake wa kuku.
KFC inasema kuku wake wanatoka katika mashamba nchini Afrika Kusini ambayo yameidhinishwa kuwa hayana homa ya mafua ya ndege.
Lesotho ni nchi ya milima iliyozungukwa kabisa na Afrika Kusini.
Afrika Kusini imekuwa ikijitahidi kudhibiti homa ya mafua ya ndege kwa miezi kadhaa na imeua zaidi ya kuku milioni saba wanaotaga mayai, 20-30% ya hisa nzima ya nchi hiyo.
Wiki iliyopita, nchi jirani ya Msumbiji ilichinja takribani kuku 45,000 walioambukizwa iliowaagiza kutoka Afrika Kusini.
Namibia pia ilipiga marufuku uagizaji wa kuku wa Afrika Kusini mwezi Septemba.
Mlipuko huo umesababisha uhaba wa mayai na nyama ya kuku katika mataifa kadhaa kusini mwa Afrika.
KFC Lesotho imewahakikishia wateja migahawa yake itafungua milango yao hivi karibuni.