Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KCBL yajinasua kufilisika ikikusanya mtaji wa Sh13 bilioni

Pic Fedha Data Wastaafu KCBL yajinasua kufilisika ikikusanya mtaji wa Sh13 bilioni

Fri, 8 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Serikali ikipambana kuirejesha sokoni Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) baada ya kuwa hatarini kufungwa, mtaji wa benki hiyo sasa umefikia Sh13 bilioni kutoka Sh1.8 bilioni waliokuwa nayo mwaka 2019.

Akizungumza jana Desemba 6, 2023 wakati wa uzinduzi wa huduma za benki kwa njia ya simu ‘KCBL Co-op mobile banking', meneja mkuu wa benki hiyo, Godfrey Ng'urah amesema kwa miaka mitatu wamepata mafanikio hayo makubwa ambayo yameleta mapinduzi makubwa katika benki hiyo.

Pamoja na mafanikio hayo, Ng'urah amesema sasa benki hiyo ina wateja wapatao 21,000 kutoka wateja 5,000 waliokuwapo mwaka 2019, huku amana za benki hiyo zikiongezeka kutoka Sh4.2 bilioni hadi Sh8.5 bilioni mwaka huu.

Amesema miaka mitatu iliyopita Serikali kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) waliomba Benki ya CRDB kufanya uwekezaji wa kimkakati wa Sh7 bilioni utakaoirejesha na kuiendesha kwa tija benki hiyo pekee ya ushirika nchini.

"Maono ya Serikali ilikuwa ni kujenga mifumo itakayosaidia benki hii kuwa endelevu, ikiwa na mifumo ya kidigitali na Tehama.

“Leo hii tuko hapa kushuhudia uzinduzi wa bidhaa mpya na bora inayoipeleka benki yetu kuwa ya kidigitali endelevu, itakayojiendesha kwa tija na kuwa benki bunifu na kuwafikia wengi kwa mara moja," amesema Ngu'urah.

Kwa upande wake, ofisa biashara kutoka Benki ya CRDB, Boma Raballa ameipongeza benki hiyo na kusema kama mwekezaji wa kimkakati ndani ya KCBL wataendelea kuwekeza na kuhakikisha malengo yote ya muda mfupi na mrefu ya uwekezaji ndani ya benki hiyo yanafanikiwa.

"Hili ni jambo la kupongezwa, kwani miaka michache iliyopita hakuna mtu angeweza kudhani benki hii ingeweza kufanya haya, watu walishaikatia tamaa, kwa sasa hongereni sana bodi ya KCBL na menejimenti,” amesema.

Naye, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Nchini, Charles Jishuli, amewataka wanachama wa vyama vya ushirika kote nchini kuendelea kuitumia benki hiyo na uongozi uhakikishe huduma zinazopatikana ndani ya benki hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live