Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jipya laibuka sakata la nguo za ndani za mitumba

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakiwa kwenye msako wa kukamata na kuteketeza nguo za ndani za mitumba, Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) imesema haiwatambui wanaoingiza bidhaa hizo nchini.

Mwenyekiti wa JWT, Silver Siondo alisema hayo jana alipozungumza na Mwananchi.

Siondo alisema wafanyabiashara wanaotambuliwa na jukwaa hilo wanatakiwa kuwa na leseni na kufuata sheria na kanuni za nchi.

“Hao hawana leseni na hawajajisajili kwetu, hivyo hatuwafahamu. Hapa kila mfanyabiashara ambaye ni mwanachama wetu akipata tatizo lazima tumsaidie, “ alisema Siondo.

“Lakini hao wanaokamatwa hawajawahi kuja kwetu kwa sababu si wanachama wetu.”

Kauli hiyo ya Siondo imekuja kutokana na operesheni inayoendelea kufanywa na maofisa wa TBS ya kukamata mitumba ya nguo hizo.

Alisema JWT haihusiki na kila mfanyabiashara anayepata tatizo, bali kigezo chao ni mwanachama kuwa na leseni ya biashara pamoja na namba ya mlipakodi (TIN).

Serikali ilizuia uingizaji wa mitumba ya nguo za ndani siku nyingi, hivyo kuendelea kupatikana kwake sokoni ni suala linalokiuka sheria na kanuni za biashara zilizopo.

Wiki iliyopita TBS ilianza kuziondoa sokoni nguo za ndani kwa kufanya msako wa ghafla kwenye soko la Tandika jijini Dar es Salaam.

Mkaguzi wa shirika hilo, Emmanuel Simon alisema huo ni mkakati wa kuhakikisha nguo hizo hazitumiwi na Watanzania na hatua hiyo ni endelevu kwa sababu mavazi hayo yanaweza kusababisha saratani na magonjwa ya ngozi.

“Utekelezaji huu ni kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Viwango ya mwaka 2009 inayozuia matumizi ya nguo za ndani za mitumba,” alisema Simon.

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema kwa kawaida huwa hawafungui makontena yenye mizigo ya nguo ili kuyakagua, bali wanachozingatia ni ulipwaji wa kodi.

“Ni vigumu kugundua nguo zilizomo kwenye kontena ni za aina gani kwa sababu, kwa kawaida hatuwezi kuzifungua, ila tunajua tu kwamba ni nguo za mitumba na kuchukua kodi yetu,” alisema Kayombo.

Afrika Mashariki

Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walipokutana jijini Arusha, Machi 2016 walipitisha azimio la kupunguza uingizaji wa nguo za mitumba na bidhaa za ngozi wakihamasisha uwekezaji wa ndani.

Viongozi hao walijipa muda wa miaka mitatu ya mkakati wa kupunguza uingizaji wa nguo hizo huku wakijipanga kuongeza uzalishaji wa nguo kwenye nchi wanachama kabla ya kuanza kuweka masharti ya kibiashara.

Chanzo: mwananchi.co.tz