Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi watu 6,500 wanavyojiingizia kipato ujenzi reli ya kisasa

29202 Pic+reli TanzaniaWeb

Wed, 28 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kilosa. Zaidi ya watu 6,500 wanaendesha maisha yao kupitia ujira wanaolipwa katika mradi wa ujenzi mpya wa reli ya Standard Gauge (SGR).

Kuna washika vibendera vya kuongozea magari, madereva wa malori, mashine kama bulldozer, mameneja waaandamizi wa uendeshaji ambao wako eneo la mradi kwenye awamu zote mbili.

Meneja wa mradi huo awamu ya kwanza kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro, Machibya Masanja aliwaambia waandishi wa habari waliotembelea ujenzi huo kuwa wana mitambo zaidi ya 1,600 kwenye mradi mzima kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma ikiwa inafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa muda kama ulivyopangwa.

“Tuna malori, magari ya kawaida, makatapila, mashine za kushindilia, kuchimba udongo na zote hizo zinaendeshwa na watu hivyo unaweza kuona ni watu wengi kiasi gani wako kwenye ‘ground’ wanafanya kazi,” alisema Masanja.

Meneja mradi awamu ya pili wa kampuni ya Yapi Merkezi kuanzia Morogoro hadi Makutuporo Dodoma, Dk Husnu Uysal alisema wameajiri watumishi wa ofisini wazawa asilimia 36.88 na wataalamu kutoka nje asilimia 63.12.

Alisema wafanyakazi wazawa wasio wa ofisini waliopo kwenye ujenzi ni asilimia 86.45 na wataalamu toka nje ni asilimia 13.55.

“Kwa ujumla tuna asilimia 72.68 ya wazawa kwenye mradi na asilimia 28.32 ya wataalamu kutoka nje hivyo ni sawa na kusema tuna wataalamu kutoka nje 291 kwenye mradi na wazawa 1,533 hiyo inafanya jumla ya wafanyakazi wote kuwa 1,924,” alisema.

Alisema wana mashine mbalimbali kama malori, makatapila na mengineyo 385 na mashine nyingine 220 zitaongezeka ifikapo Desemba ili kwenda na kasi ya kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa.

Mhandisi wa Shirika la Reli Tanzania(TRC), Faustine Kataraiya anayesimamia awamu ya pili kuanzia Morogoro hadi Dodoma alisema kuna ujenzi wa kilomita 86 ya njia za mapishano na kilomita 336 ya njia kuu.

“Kazi kubwa imeanza mwezi wa pili, tuna miezi 36 mradi kukamilika, sasa hivi tunafanya ukataji wa udongo usiohitajika ili kusafisha barabara,” alisema na kuongeza kuwa wanakata udongo hadi mita nne kwenda chini na kujaza kifusi kizuri kwa ajili ya uimara wa reli.

Alisema pia wanajenga njia ya umeme ya KV 220 na kutakuwa na vituo saba vya kupoozea umeme huo ili ufikie KV25 ambayo ndiyo itatumika kuendeshea treni.

Kataraiya alisema katika eneo la Makutupora hadi Gulwe, kuna vilima hivyo kuna kazi ya kuvichonga na kutoboa matobo manne yenye kilomita mbili.

“Kwa upande wa hapa Kilosa kuna vilima pia, hivyo kuna eneo inabidi tutoboe mlima urefu wa kilomita 2.5 ambako reli itapita kwenye tobo hilo. Ni kazi kubwa inahitaji utaalamu wa hali ya juu,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz