Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi wakulima wanavyoibiwa na madalali Dar

37533 Wakulima+pic Jinsi wakulima wanavyoibiwa na madalali Dar

Tue, 22 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakulima wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali katika shughuli zao kuanzia kulima, upandaji wa mazao na pembejeo.

Kwa wale wakulima wa mazao ya biashara kilio chao kingine ni utapeli, wizi na wakati mwingine kudhulumiwa fedha na madalali wasio waaminifu wanapofika sokoni. Katika makala haya, mwandishi wetu anaangalia namna wakulima wanavyoibiwa katika masoko ya Dar es Salaam. Sasa endelea...

Alipoamua kuzamisha Sh950,000 kwenye kilimo cha matikiti Kijiji cha Kijaka, Manispaa ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Mohamed Juma (26) aliamini kuwa angeuza mazao yake sokoni kwa bei yenye faida kubwa.

Kwa msukumo huo, Juma aliamua kuelekeza nguvu zake zote kuhudumia shamba lake lenye ukubwa wa eka tatu. Alihakikisha mazao yake yanapata maji wakati wote.

Ulipofika wakati wa kupalilia, hakusita kuajiri na kuwalipa vibarua kumfanyia kazi hiyo. Baadaye akaingia tena mfukoni kununua dawa za kuua wadudu waharibifu, tumaini lake likiwa lilelile—atakapouza matikiti atarudisha gharama na kupata faida.

Miezi sita imetimia na matikiti yamekomaa tayari kupelekwa sokoni. Awali, alijua wanunuzi wangejitokeza na kununulia ‘mzigo shambani (madalali wa shambani) ili kuepuka kuharibika yakiwa huko. Hata hivyo, hilo halikutokea.

Juma alilazimika kwenda mwenyewe mjini kutafuta soko na uwezekano wa kusafirisha mzigo wake kuupeleka sokoni.

Alianza kwa kuzungukia soko la Ilala, baadaye akaenda lile la Tandika ambapo alimpata dalali wa soko la Buguruni aliyekubali kwenda kuangalia mzigo shambani ili akiridhika nao aupeleke sokoni.

Mapema asubuhi siku iliyofuata, dalali huyo alikubali kwenda na Juma hadi kijijini Kijaka, aliridhika na mzigo na walipatana kuwa atalipia gharama za usafiri ambazo watarudishiana baada ya kukamilisha mauzo.

Gari aina ya Mitsubishi Canter lenye uwezo wa kubeba tani tatu linalobeba mzigo kwa Sh200,000 hadi sokoni, lilipatikana. Dalali alilikodi, wakaingia sokoni Buguruni saa tano usiku na kukuta magari mengine yakishusha matikiti. Walisubiri hadi saa saba wakaanza kushusha na ilipofika saa tisa alfajiri walikuwa wamemaliza.

Hapa Juma alielezwa kuwa kutakuwa na gharama ya Sh49,000 ya ulinzi wa soko, usafi pamoja na kushusha mzigo. Kwa kuwa hakuwa fedha, dalali alilipa pia gharama hizo. Hadi kazi ya kushusha ilipomalizika hesabu zilionyesha kuwa matikiti 1,840 yenye ukubwa tofauti yalikuwa yameshushwa.

Maumivu yaanza

Katika hatua hii ndipo Juma alipoanza kuhisi maumivu baada ya dalali kumweleza kuwa kwa kawaida huwa wanatoza Sh200 kwa kila tunda, akimanisha kuwa atalazimika kumlipa Sh386,000 baada ya mauzo.

Hata hivyo, baada ya Juma kutaka maelezo zaidi, dalali alikuja na utaratibu mwingine akimweleza kuwa fedha hizo zitalipia gharama za kukodi maturubai mawili - moja la kuwekea mzigo na lingine la kufunikia.

Juma anasema gharama zile zilimuumiza kwa kuwa kati ya matikiti yake 1,840, ni 600 pekee yangeweza kuuzwa kwa zaidi ya Sh1,000. Katika hesabu hii, matunda yaliyooza au kupasuka wakati wa kuhesabu yalijumuishwa.

Mpaka saa tisa alfajiri walimaliza kushusha na kufanya makubaliano wakutane kesho yake saa 11 alfajiri.

Hata hivyo, Juma alilazimika kulala sokoni hapo kwa kuwa muda ule asingeweza kwenda kokote.

“Hali ilikuwa mbaya zaidi wakati wa kuuza kwani matunda ambayo mwanzo aliniahidi (dalali) tungeuza kuanzia Sh5,000 tuliuza kwa Sh4,000 tu, na yeye ndiye aliyekuwa akiamua bei akidai kwamba siku hiyo kulikuwa na matikiti mengi sokoni hivyo tusipouza chini ya bei yangelala,” alilalamika katika mahojiano na Mwananchi.

Juma anasema ilipofika saa 6:30, wakiwa wamebaki na theluthi moja ya mzigo, dalali alianza kumshawishi wauuze wote kwa ujumla.

“Alinilazimisha akidai matikiti yameshikwashikwa sana na kama yangelala kesho yake yangeuzwa kwa bei ya chini zaidi. Baada ya kuvumilia mpaka saa nane mchana nilichoka, niliamua kukubaliana naye.”

Katika hatua hii, Juma alikubali kuuza mzigo wote uliobaki kwa Sh240,000.

“Kwa sababu nilikuwa nakusanya fedha aliniambia nihesabu na nimpe kabisa pesa yake,” alieleza Juma ambaye pia ni mhitimu wa stashahada teknolojia ya maabara (maji).

Baada ya biashara, Juma alijikuta akiambulia Sh1,320,500.

“Niliumia sana kwani baada ya kumlipa fedha zake (dalali) na madeni mengine aliyokuwa ananidai nilibaki na Sh685,500.”

Anasema, masikitiko yake yanatokana na kutumia gharama kubwa kwa kilimo, lakini alichoambulia kiliishia kumkata mtaji alioutumia.

Mwisho wa siku aliondoka na hasara ya Sh264,500 huku dalali akitia mfukoni Sh386,000 kwa kazi ya siku mbili.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa kilichompata mkulima huyo ni kilio cha maelfu ya wakulima wa matunda na nafaka nchini ambao hatima ya biashara zao hivi sasa inaamuliwa na madalali.

Allen Saria, mkulima na muuzaji wa matunda anasema alishawishiwa na dalali auze matenga yake 77 ya ndizi mbivu kwa Sh20,000 kila moja baada ya kumwaminisha kuwa hali ya soko ilikuwa mbaya kipindi hicho.

Japo Saria alipanga kuuza kwa bei ya juu ilibidi akubaliane na bei ya dalali akiogopa kuharibika kwa matunda yake.

“Aliniambia tutauza kwa Sh20,000 lakini nilishangaa akiuza hadi Sh35, 000 kwa tenga,” anaeleza mkulima huyo.

Baada ya mzigo kwisha dalali alimkabidhi Sh1,540,000 zilizotokana na mauzo ya matenga 77 kwa Sh20,000 kwa kila tenga .

“Kwa kweli nilisikitika kwani nilishuhudia akiuza hadi Sh35,000 kwa tenga.”

Serikali inasemaje?

Kaimu mkurugenzi wa Idara ya Masoko katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Wilson Malosha anasema changamoto wanayopata wakulima mikononi mwa madalali ni wito muhimu kwao kujiunga katika vyama vyao ili waweze kujitafutia masoko ya uhakika na kusimamia bei zao.

“Kuna haja ya wakulima kuacha kufanya mambo kienyeji. Ni vizuri wakajiunga kwenye vyama kama ilivyo kwa wakulima wa maparachichi, alizeti na wengine,” anasema Malosha.

Anasema, “Takwimu zinaonyesha wote waliojiunga kwenye umoja wa wazalishaji zao fulani wamefanikiwa kupata masoko hadi nje ya nchi na kujiongezea nguvu ya kupatana sokoni na kuwakwepa madalali.”

Anatoa wito kwa viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali wanaosimamia masoko kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha madalali wasiosajiliwa hawawabughudhi wakulima.

Pia, anasema kila wizara hukusanya wastani wa bei za mazao mbalimbali nchi nzima na kuzitangaza ili kuwashtua wanunuzi na wauzaji wasije kulanguliwa.

“Hata madalali hawatakiwi kwenda nje ya soko. Huwa tunatoa taarifa za bei za bidhaa ili kuepusha watu kupandisha ama kushusha bei kiholela kwa masilahi ya upande fulani,” anasema.

Anawataka wakulima kuendeleza utamaduni wa kuzingatia kuuza mazao katika vipimo vinavyoeleweka ili kuepuka kupangiwa bei na madalali.

“Tunataka bidhaa zote ziuzwe kwa vipimo sahihi na siyo kutumia ndoo au lumbesa au makopo. Sasa kupitia taasisi yetu ya vipimo tunataka tuwe na vituo maalumu ya kuuzia mazao.”

Anasema, kwa mfano halmashauri inaweza kutambua eneo kwa ajili ya wakulima wa nyanya au vitunguu, kwa hiyo kupitia chama chao wakapeleka mazao kwenye vituo hivyo. Mizigo ikiingia inafungwa katika vipimo vinavyokubalika (ili) kurahisisha uuzaji na kuepuka kupangiwa bei.”

Namna gani viongozi wa masoko wanavyowalinda wakulima na madalali, usikose sehemu inayofuata kesho



Chanzo: mwananchi.co.tz