Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi upanuzi Bandari ya Dar unavyolipa

9cb5e9c778d8dc38451649ee79f53455.jpeg Jinsi upanuzi Bandari ya Dar unavyolipa

Tue, 28 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Akiwa na uso wenye tabasamu kubwa huku akiwa amesimama kwa madaha katika maeneo salama ya Bandari ya Dar es Salaam, mfanyabiashara Aziz Salim anasema upanuzi wa Bandari hiyo umeleta nafuu kubwa katika biashara zake.

Salim alikuwa akishuhudia kupakuliwa kwa ngano aliyoiagiza kutoka ughaibuni iliyokuwa ndani ya meli ya MV Red Orchid ambayo kwa wakati huo ilikuwa imetia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam. “Kuangalia shehena yangu ikishushwa kwa mkupuo hapa bandarini kunanifariji sana, kwa sababu hapo awali meli kubwa kama hiyo haikuweza kutia nanga hapa, na meli hii inabeba zaidi ya tani 50,000 za nafaka,” anasema Salim.

Salim ambaye anafanya biashara za ngano kwa muda mrefu, alisema alikuwa na shida sana ya kuingiza mzigo wake katika siku za nyuma kutokana na uwezo wa bandari, kwenye kuruhusu meli kubwa kuingia na kushusha shehena kubwa. Lakini anasema tangu Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuanza mradi wa upanuzi wa bandari mambo mengi yamekuwa yakibadilika na kuifanya bandari hiyo kuwa shindani na bandari nyingine.

“Zamani meli kubwa hazikuweza kutia nanga kwenye gati namba moja hadi tatu, lakini sasa meli kubwa zinaweza kutia nanga bila kikwazo chochote na kupakua shehena kubwa kama shehena yangu ninayopakua,” anasema Salim. Akipokea shehena hiyo, Kaimu Meneja anayeshughulikia masuala ya nafaka wa TPA, Tatu Moyo anasema amefurahishwa sana na ujio wa meli hiyo iliyokuwa na tani 50,596 za ngano.

Anasema meli hiyo ambayo ilibeba shehena kubwa ya nafaka ambayo haijawahi kurekodiwa bandarini hapo akihusisha na mradi wa upanuzi wa bandari. Tatu anasema meli hiyo iliweza kutia nanga kwenye gati kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali katika bandari hiyo kwa thamani ya dola za Marekani milioni 421.

Mradi huo ambao umeanza kutekelezwa tangu mwaka 2017 kwa lengo la kuboresha ufanisi Bandari ya Dar es Salaam umeimarisha uwezo wa kitaasisi wa TPA na bandari zake. Anasema kabla ya utekelezaji wa mradi huo, gati ilikuwa na uwezo wa kuingiza meli zenye uwezo wa kubeba tani 30,000 pekee, lakini sasa meli kubwa zaidi zinaweza kutia nanga bila changamoto.

Ikifadhiliwa na serikali ya Tanzania kwa pamoja na Benki ya Dunia na Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza, mradi huo unaotambulika kama DMGP umesaidia kuongeza kina kutoka mita 1-7 hadi 14.5.

“Kwa ongezeko hili bandari sasa inaweza kupokea meli kubwa kwa urahisi, ikilinganishwa na hali ya awali ambapo kina kilikuwa ni mita nane. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi, mipango iko mbioni kuhakikisha maboresho yanafanyika kwenye kina sanjari na gati namba 8-11.

Pamoja na kuboresha gati na kina hadi mita 15.5 na huku ikipanua njia ya kuingilia na kugeuza meli hadi gati 11, mradi huo pia umelenga kuboresha maunganisho ya uchukuzi kati ya bandari na reli. Anasema uboreshaji wa miundombinu katika bandari hiyo kumechochea ufanisi ambapo kwa mwaka huu pekee katika kipindi cha miezi miwili bandari hiyo ilipokea magari zaidi ya 8,000 kupitia MV Frontier Ace yenye jumla ya magari 4,041 na baadaye kuwasili kwa MV Meridian Ace na shehena ya magari 4,397.

“Upakiaji wa meli moja moja ulikamilika ndani ya saa 17 baada ya kuwasili, ambayo ni sawa na magari matatu kwa dakika. Hapo awali, upakiaji wa magari 300 pekee ungechukua hadi saa 34,” anasema Hamissi. Hamissi anaendelea kusema kuwa TPA imepiga hatua kubwa katika kuongeza ufanisi katika bandari zake, hasa bandari ya Dar es Salaam ambayo inahudumia takribani asilimia 95 ya mizigo ya kimataifa ya Tanzania na nchi jirani za Burundi, Rwanda, DRC, Zambia na Uganda.

Anasema TPA katika utendaji wake imedhamiria pia kuhakikisha bandari inaendelea kutoa huduma bora ili kuvutia wateja wapya pamoja na kuwarejesha wateja wa zamani ambao kwa sababu moja au nyingine waliamua kutotumia bandari hiyo. Bosi huyo wa TPA kwa upande wake anasema kwamba anaishukuru serikali kwa kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha miundombinu ya bandari, kupata vifaa vya kisasa, teknolojia na utaalamu.

Mkurugenzi Mkuu huyo anaongeza zaidi kuwa, mbali na kupokea shehena kubwa ya magari na mizigo mingine katika historia ya bandari hiyo, uboreshaji wa bandari hiyo umeongeza ufanisi, ambapo Novemba mwaka jana Mamlaka hiyo ilivunja rekodi nyingine kwa kuhudumia meli 77 za mizigo na makontena 7,000, ambayo yamevuka lengo lao la kila mwezi la kupokea kontena 10,000 kwa mwezi.

Bandari ya Dar es Salaam inahudumia nchi zisizo na bandari za Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi, Rwanda na Uganda. Bandari hii imewekwa kimkakati ili kutumika kama kiunganishi cha kubeba mizigo kwa urahisi sio tu kwenda na kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati bali pia Mashariki ya Kati na ya Mbali, Ulaya, Australia na Amerika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live