Mkutano wa 221 wa Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (MPC) umethibitisha kuashiria cha uwezekano wa ongezeko la mfumuko wa bei nchini kwa siku za usoni kutokana na kasi kubwa ya kuendelea kuongezeka bei za chakula, nishati na mbolea katika soko la dunia.
Tahadhari hiyo inatolewa ikiwa ni miezi kadhaa tangu ulipofanyika uchambuzi wa changamoto ya kupanda kwa bei ya bidhaa katika maeneo ya mikoa mbalimbali, wananchi wakilia maumivu ya bei.
Kwa mujibu wa BOT, mfumuko huo uliongezeka hadi asilimia nne Mei kabla ya kupanda hadi asilimia 4.4 Juni mwaka huu kutokana na upandaji wa bei za bidhaa zinazotoka nje ya nchi licha ya kubakia ndani ya lengo la asilimia wastani wa asilimia tatu hadi tano kwa Tanzania Bara na asilimia tano kwa Zanzibar.
“Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha, uliopelekea kuwepo ukwasi wa kutosha katika mabenki, na hivyo kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi,”ilinukuliwa katika sehemu ya taarifa ya juzi ya kamati hiyo chini ya mwenyekiti wake, Gavana wa BOT, Profesa Florens Luoga.
“Hata hivyo kamati imeendelea kufuatilia kwa karibu ongezeko la mfumuko wa bei kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, hali ambayo inaweza kuathiri kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.”
Kikao hicho kilichotathmini utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi kwa Mei na Juni 2022 kamati iliridhia BOT kupunguza kasi ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi katika nusu ya pili ya mwaka huu ili kukabiliana na athari za ongezeko la mfumuko wa bei, bila kuathiri kasi ya ukuaji wa uchumi.
Pili, kamati hiyo ilisisitiza umuhimu wa BOT kuendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni ili kuendelea kuimarisha utulivu wa thamani ya shilingi na kulinda uchumi dhidi ya athari za kuongezeka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia.
Uchumi wa dunia
Katika taarifa hiyo Profesa Luoga alisema uchumi wa dunia umeendelea kukabiliwa na athari za vita nchini Ukraine, kuibuka upya kwa maambukizi ya ugonjwa wa Uviko-19 nchini China, ongezeko la mfumuko wa bei, pamoja na mazingira magumu ya kifedha katika soko la dunia.
“Athari hizo ziliendelea kudumaza kasi ya kuimarika kwa uchumi wa dunia na hivyo kupelekea Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kushusha makadirio ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2022 na 2023, ikilinganishwa na makadirio ya awali,”alinukuliwa