Dar es Salaam. Uongozi wa Jiji la Dar es Salaam umesema una fedha za kununua mabasi 100 ya mwendokasi na kuyaingiza barabarani iwapo Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) itawapa kibali.
Hayo yamesemwa jana Jumatano Aprili 10, 2019 na meya wa jiji hilo, Isaya Mwita baada ya kupokea ugeni wa Bodi ya ya Jiji la Kisumu nchini Kenya waliopo nchini kujifunza kuhusu mradi huo.
Mwita amesema changamoto iliyopo katika usafiri wa mabasi yaendayo haraka itatatuliwa na jiji iwapo tu Wizara ya Tamisema itatoa kibali cha kuendesha mradi huo.
“Kwetu sisi kama jiji tuna fedha za kuendesha huo mradi na tunaamini hata kama hatutamaliza changamoto lakini tutasaidia kuondoa adha ya usafiri wanayopata wananchi,” amesema Mwita na kuongeza:
“Pia, niwaombe radhi wananchi ambao wanapata tabu na usafiri huo kwa kuwa hata jiji halifurahishwi ndio maana hata sisi tunataka tuingie katika biashara hiyo.
“Huu mradi ni wakisasa ndio maana wenzetu wamekuja kujifunza kutoka kwetu, niwaombe radhi wananchi kutokana na adha hiyo wanayoipata ila baada ya kipindi kifupi haitajitokeza tena.”
Naye mwenyekiti wa bodi ya Kisumu, Elijah Onyango, amesema katika ziara hiyo ameongozana na watu 27 huku moja ya vitu vilivyowavutia ni mradi wa mabasi hayo.