Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Je wajua kuwa asilimia 36.2 ya bajeti itagharamia miradi?

Mwigulu Uchumi Kupungua.png Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha

Wed, 15 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali inakadiria kutumia Sh trilioni 15.005 sawa na asilimia 36.2 ya bajeti yote ya serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 kugharamia miradi ya maendeleo ikijumuisha ya huduma za jamii. Haya yalielezwa bungeni Jumanne na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2022/23.

Alisema kati ya kiasi hicho, Sh bilioni 12,305.8 sawa na asilimia 82 ya bajeti ya maendeleo ni fedha za ndani na Sh bilioni 2,699.1 sawa na asilimia 18 ni fedha za nje. Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23 ni wa pili katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) wenye dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Dk Mwigulu alisema katika kuongeza ukusanyaji wa mapato ya kugharamia mpango huo, serikali itaweka mikakati ya kusimamia ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani, kuimarisha mfumo wa kielektroniki wa kufuatilia mizigo inayokwenda nchi jirani, kuimarisha ushirikiano na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo zinapatikana kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali nchini.

Kwa upande wa ugharamiaji wa miradi ya maendeleo itakayotekelezwa kwa utaratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), alisema serikali imepanga kuwezesha mamlaka za serikali zenye miradi ya PPP iliyopo katika hatua mbalimbali za maandalizi ikiwamo upembuzi yakinifu na ununuzi wa wabia kukamilisha miradi hiyo iweze kuanza utekelezaji.

Malengo na Shabaha

Dk Mwigulu alisema malengo na shabaha ya ukuaji wa uchumi katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 ni ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 4.7 mwaka 2022 na asilimia 5.3 mwaka 2023 na kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 hadi 7.0 katika muda wa kati.

Alisema pia mapato ya ndani kufikia asilimia 14.9 ya Pato la Taifa, mapato ya kodi kufikia asilimia 11.7 ya Pato la Taifa, kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

Miradi ya kipaumbele

Dk Mwigulu alisema serikali itaendelea kukamilisha miradi ya kielelezo na ya kimkakati inayoendelea itakayoleta matokeo mapana na ya haraka katika uchumi ikiwamo kuzalisha ajira, kipato na kuchangia zaidi kupunguza hali ya umaskini nchini.

Alisema miradi ya kipaumbele itazingatia maeneo matano ya kipaumbele ambayo ni, kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na huduma, kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.

Vihatarishi

Alisema utekelezaji wa mpango huo unaweza kuathiriwa na vihatarishi vya ndani na nje, ikiwamo ufinyu wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na mitikisiko ya kiuchumi duniani.

Alisema katika kukabiliana na vihatarishi hivyo, serikali itaimarisha ukusanyaji na usimamizi wa kodi, kuhamasisha ulipaji kodi katika sekta isiyo rasmi kwa kuijumuisha kwenye mfumo rasmi wa ulipaji kodi na kuendelea kuweka mazingira ya kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi wa ndani na nje ili kupunguza gharama za uwekezaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live