Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Japan yaisaidia TRA vifaa kuzuia upotevu mapato

JAPAN Japan yaisaidia TRA vifaa kuzuia upotevu mapato

Wed, 26 Jan 2022 Chanzo: ippmedia.com

Serikali ya Japan kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la maedeleo la nchini humo JICA, limeipatia Tanzania kupitia Mamlaka ya Mapato nchini TRA msaada wa vifaa mbalimbali yakiwemo magari matatu pamoja na boti za kisasa zitakazosaidia kupunguza upotevu wa mapato.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, alisema magari hayo yatasaidia kuimarisha doria kwenye mikoa ambayo ina biashara za magendo kwa wingi.

Aliitaja mikoa ambayo magari hayo yatapelekwa ikiwamo Dar es Salaam, mpaka wa Kasumulu mkoani Mbeya na Tunduma mkoani Ruvuma pamoja na boti ambayo itakuwa ikifanya doria ya kudhibiti magendo katika Bahari ya Hindi, na kusisitiza kuwapo upotevu wa mapato mengi katika ukanda huo.

“Wote tunafahamu tunapoteza mapato mengi kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi, hivyo tumepatiwa boti nzuri inayoenda kasi ambayo itatusaidia kulinda mpaka katika eneo hilo, lakini wametupatia kifaa kinachotumika kukagua mizigo (X-ray baggage scanner).

“Kifaa hicho tayari kimeshasimikwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA), kazi kubwa ni kudhibiti mizigo ya mikononi ili kufahamu kilichomo na kuhakikisha mapato ya serikali hayapotei,” alisema Kidata.

Pia alisema vifaa vingine vilivyotolewa ni pamoja na vya kugundua dawa za kulevya (Drug detection kits) ambavyo vitasaidia kuzuia upitishaji wa dawa hizo nchini na (Portable Raman Spectrometer) ambayo ni kwa ajili ya kutambua dawa za kulevya na vilipuzi ndani na nje ya jengo.

Alisema dhumuni la msaada huo ni katika kuhakikisha kwamba (TRA) inapata mapato yake halali na kuzuia uvujaji wa mapato ambao unatokana na biashara za magendo, pia kuhakikisha kwamba afya za Watanzania zinalindwa kwa kuzuia dawa za kulevya.

Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini Goto Shinichi, alisema msaada wa vifaa hivyo umelenga kusaidia katika kukuza zaidi maendeleo ya uchumi wa kikanda kupitia uwezeshaji kibiashara na udhibiti salama wa mipaka.

 

“Hii itasaidia kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na Japan, lakini kuchochea maendeleo ya kiuchumi kijamii, kikanda na bara, wakati huo huo, usimamizi mzuri wa mipaka pia utazingatiwa katika kudhibiti wahalifu wa kuvuka mipaka kama vile magendo na kuchukua hatua dhidi ya kuenea kwa COVID-19,” alisema Shinichi.

Chanzo: ippmedia.com