Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

January aeleza utekelezaji maazimio ya COP26 nchini

Dc4cbded138b44d42c0da8f4df032b04.jpeg January aeleza utekelezaji maazimio ya COP26 nchini

Sat, 25 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Nishati, January Makamba (pichani) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi, Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika, Janet Rogan kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano wa viongozi hao ulifanyika jijini Dodoma juzi na kuhudhuriwa na Balozi wa Uingereza nchini, David Concar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali pamoja na watendaji wengine kutoka ubalozi wa Uingereza nchini.

Majadiliano ya viongozi hao yalihusu mabadiliko ya tabianchi pamoja na Tanzania ilivyojipanga kutekeleza maazimio ya Mkutano wa 26 wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP26) uliofanyika mwaka 2021 nchini Uingereza. Baadhi ya maazimio ya mkutano huo ni pamoja na uhamasishaji wa matumizi ya nishati mbadala, matumizi ya umeme kwenye magari pamoja na kupunguza ukataji miti.

Katika mazungumzo hayo, January alimweleza Rogan kuwa Tanzania inafanya juhudi mbalimbali kutekeleza maazimio hayo kwa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala mijini na vijijini pamoja na magari kutumia gesi asilia na umeme. January alieleza juhudi zinazofanywa na serikali katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na nishati ya kutosha kwa kuendeleza vyanzo mbalimbali vya nishati ikiwamo jotoardhi, jua na gesi asilia.

Pia alisema serikali ipo katika mpango wa kuandaa na kuboresha mikakati mbalimbali ya kisekta pamoja na kuboresha mfumo wa gridi ya taifa ili kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na nishati ya uhakika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live