Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jamii yatakiwa kutokwepa kulipa kodi

Cdb80576c4fc1fdd3cab7dcfb7e34589 Jamii yatakiwa kutokwepa kulipa kodi

Mon, 20 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JAMII imeshauriwa kuacha kukwepa kulipa kodi ili kusaidia upatikanaji wa huduma za msingi ikiwemo ujenzi wa shule, kuondoa tatizo la watoto kusoma chini ya miti kwenye shule.

Ushauri huo ulitolewa na Meneja Miradi ya Elimu Shirika lisilo la Kiserikali la ActionAid Tanzania, Karoli Kadeghe katika mkutano wa wadau wa kujadili hali ya upatikanaji wa elimu jumuishi Wilaya ya Chamwino, Dodoma.

Elimu Jumuishi inapatikana kwa msaada wa Action- Aid kupitia mradi wa elimu wa ‘Kuondoa Vikwazo, haki-kodi na huduma za jamii zinazozingatia jinsia na mahitaji maalumu’ unaofadhiliwa Shirika la Maendeleo Norad. Kadeghe alibainisha kuna wakati jamii inakwepa kodi bila kujua.

“Hata tunaposafiri tunanunua chakula na watu hatudai risiti na usipodai ina maana umemuachia fedha za kodi mwenye hoteli na hatawasilisha serikali, na pia tufuatilie kodi yetu imefanya nini hasa kwenye huduma za msingi kama elimu, afya na maji”.

Alisema baadhi ya shule zina uhaba wa vyumba vya madarasa na wanafunzi husomea chini ya miti, hivyo jamii ina wajibu wa kuisaidia serikali kuhakikisha inapata mapato ya kutosha na kufuatilia kwa kina matumizi ya kodi zao.

“Tungependa kuona wana jamii wanafuatilia fedha za serikali ambazo ni zao zinazotumwa shule ili kutimiza utoaji wa elimu,”alisema.

Alisema kupitia mradi huo, kamati za shule na wazazi zinafuatilia madarasa yajengwe ili kuondokana na watoto kusoma chini ya mti.

“Pale shule ya msingi Mahama wanasomea chini ya mti. Sasa vimejengwa vyumba vitatu inaonesha kamati za shule zimefikisha changamoto shuleni kwa viongozi wa kijiji na kuchukua hatua serikali imejenga,” alisema.

Aidha, alisema baadhi ya shule zimeweka vyumba kwa watoto wa kike ili kujistiri wanapokuwa hedhi wasikose masomo yao. Akizungumzia mradi huo ulioanza Julai 2018 Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma na Singida, alisema unatekelezwa shule 17 za msingi na tatu za sekondari na utakamilika Desemba 2021 unagharimu Sh bilioni 1.4.

Aidha alisema lengo la mradi huo ni kuondoa vikwazo kwa watoto wa kike wenye mahitaji maalumu wapate elimu bora na jumuishi.

“Tunafanya kazi na kamati za shule kujengea uwezo wasimamizi ubora wa elimu walio karibu na jamii na klabu za watoto shuleni wajue haki zao za msingi kupata elimu bora,” alisema.

Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Mahama, Nola Elia alisema, kupitia mradi huo wamepata maboma matatu na kuondoa uhaba wa madarasa. Awali watoto walisomea chini ya mti.

Chanzo: habarileo.co.tz