Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jafo atoa miezi 2 usalama wa salfa

73d5327bbfa2575c723faf2d1c6b31a3.jpeg Jafo atoa miezi 2 usalama wa salfa

Mon, 28 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KAMPUNI ya Dar es Salaam Corridor Group (DCG), iliyoanza kupakua shehena ya salfa katika Bandari ya Dar es Salaam, imeagizwa kukamilisha taratibu za kiusalama ndani ya miezi miwili ili ipate cheti kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (​NEMC).

Kampuni hiyo imetakiwa ndani ya kipindi hicho, iwe imekamilisha tathmini ya usalama wa mazingira na ihakikishe bidhaa inazopakua hazileti athari kwa mazingira.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo, alitoa agizo hilo jana alipotembelea na kukagua upakuaji wa mzigo huo wa salfa na ghala la kuhifadhia mzigo huo katika bandari hiyo mkoani Dar es Salaam.

Alisema kampuni ya CDG ilikuwa inashughulikia shehena ya mbolea ,lakini sasa imeanza kupokea oda za kupakua shehena ya salfa, hivyo inapaswa kuwa na cheti cha NEMC

“Sasa mchakato wa kupata cheki hiki ulikuwa bado haujakamilika ndio maana leo (jana) nimekuja hapa. Kwa upande wetu ilibidi tuzuie kabisa kwa sababu hamna cheti cha mazingira, lakini tunafahamu mzigo tayari umekuja kwa maslahi mapana ya nchi yetu,” alisema Jafo.

Alisema watalaamu wa mazingira walitoa maelekezo juu ya nini cha kufanya katika eneo la ghala ili kushughulikia salfa ikizingatiwa kuwa, ghala hilo pia lilikuwa linahifadhia mbolea.

“Nawataka CDG mzingatie maelekezo yote yaliyotolewa na taasisi ya NEMC jinsi gani katika utaratibu huu mpya, mtaweza kukidhi matakwa ya mazingira katika utunzaji wa salfa na mbolea,” alisema Jafo.

Alisema katika uangalizi wa bidhaa hiyo, serikali imeipatia kampuni hiyo muda maalumu kuhakikisha salfa inaposhushwa na kupakiwa kwa ajili ya kusafirishwa, iende salama bila kuathiri mazingira.

Aliitaka kampuni hiyo ifanye kwa karibu zaidi ukaguzi na usalama wa mazingira kwa kuwa uingizaji wa salfa hiyo uko chini ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, mbolea iko chini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na suala la mazingira liko chini ya NEMC.

“Ninafahamu kuwa msipoweka utaratibu mzuri wa kushughulikia bidhaa hizi mbili mbolea na salfa, zinaweza kuleta shida kubwa ikiwemo kuathiri udongo hapo baadaye,” alisema Jafo.

Aliagiza timu ya ukaguzi kutoka NEMC kusimamia ushushaji wa safla hiyo hadi namna inavyoshughulikiwa katika ghala hadi kusafirishwa ili kuzuia athari yoyote kwa mazingira.

“Kwa sababu nyie mnakuja upande mwingine wa biashara na kwamba upo uwezekano wa kupokea oda kutoka nchi nyingi zaidi, hili lisiwe jambo la zima moto. Ikiwezekana, wekeni maghala mengine makubwa zaidi tofauti ya salfa na mbolea ili muweze kushughulikia bidhaa hizi na kuzisafirisha vizuri,” alisema.

Alitoa changamoto kwa washauri wanaotumiwa na kampuni nchini kutoingilia na kuharibu suala la mazingira bali wahakikishe wanafanya kazi kwa weledi.

Alipongeza kwa kampuni hiyo kupokea salfa ya chembechembe na si ya unga ambayo ni rahisi kuishughulikia na kuepusha athari kubwa ikiwemo milipuko.

Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya CDG, Sada Shaban, alisema wamepokea na kuanza kupakua mzigo wa salfa ambayo ni takribani tani 1,500.

Chanzo: www.habarileo.co.tz