Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jafo: Tumieni bidhaa za hapa nchini ujenzi wa miradi

83ca38b8f0b693832e13c9c072917c54 Jafo: Tumieni bidhaa za hapa nchini ujenzi wa miradi

Thu, 23 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Nchi Ofi si ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo ameziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini katika ujenzi wa miradi mbalimbali wanayoitekeleza ikiwemo ya shule, masoko pamoja na hospitali.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea kiwanda kinachozalisha vifaa vya umeme cha Kilimanjaro Cables (Africab) jijini Dar es Salaam jana, Waziri Jafo alisema matumizi ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini vikiwemo bidhaa hizo za umeme, ni muhimu kutumika katika miradi hiyo ya serikali kutokana na ubora uliopo katika bidhaa hizo kwa sasa.

“Hakuna shaka kwamba hivi sasa viwanda vyetu kikiwemo hiki cha Africab vinafanya kazi nzuri na kubwa katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi yetu ambayo kwa sasa imeingia katika uchumi wa kati, nitoe rai kwa halmashauri zote kuhakikisha zinaunga mkono juhudi hizo kwa kununua bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu,” alisema.

Alisema matumizi ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini, pamoja na kuzingatia ubora pia vinasaidia katika kulinda fedha ya ndani ambayo ingeweza kutumika kwa kuagiza au kununua bidhaa kutoka nje ya nchi ambazo hata hivyo baadhi vimebainika kutokuwa na ubora unaotakikana.

Pia alikipongeza kiwanda hicho kwa hatua mbalimbali za utengenezaji wa bidhaa za umeme zikiwemo nyaya, mabomba (PVC) soketi pamoja na transfoma huku akisisitiza kuwa hatua hiyo imeonesha kwa dhati juhudi za Tanzania katika harakati zake za kukuza viwanda kama ilivyosisitizwa kwa nyakati tofauti na Rais John Magufuli.

“Haya ni maendeleo makubwa kwa taifa letu, tunapaswa kujisifia kwa hatua hii, kikubwa endeleeni kuzalisha bidhaa bora na zenye kukidhi matakwa ya taifa letu, huu ndiyo uzalendo wa kweli,”aliongeza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe alisema ofisi yake itahakikisha inayetekeleza maagizo ya Waziri Jafo kwa kuhakikisha ujenzi wa miradi yote ya serikali katika wilaya hiyo inatumia bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho na vingine vilivyopo nchini.

Alisema kwa uzoefu wake, anaamini bidhaa zinazozalishwa nchini nyingi huwa zenye ubora mzuri kuliko zinazoingizwa kutoka nje ya nje huku kwa pamoja wakikipongeza kiwanda hicho cha Africab kwa kutoa ajira zaidi ya 400 kwa vijana wa kitanzania na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira lililopo nchini.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa kiwanda hicho, David Tarimo alisema pamoja na uzalishaji wa bidhaa zenye ubora, kiwanda hicho kimekuwa mstari wa mbele katika kuzalisha nyaya na vifaa vingine vinavyotumika katika miradi mbalimbali ya serikali ikiwemo ile ya kimkakati.

Alisema changamoto wanayokabiliana nayo ni pamoja na uwepo wa bidhaa zisizo na ubora zinazozalishwa na baadhi ya viwanda hapa nchini na zingine kutoka nje ya nchi zisizo na ubora hatua ambayo mara nyingine imekuwa ikisababisha madhara ikiwemo nyumba kuungua.

Chanzo: habarileo.co.tz