Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jafo: Biashara hewa ya ukaa ndio mpango mzima

Hewa Ya Ukaaa Ukaa Jafo: Biashara hewa ya ukaa ndio mpango mzima

Wed, 30 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwa nini tumefika hapa? Wataalamu wa masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi wanasema ukosefu wa mvua za kutosha na kwa wakati ndio chanzo cha ukame na sababu yake kubwa ni mabadiliko ya tabianchi.

Shughuli za kibinadamu zinatajwa kuwa chanzo kikubwa cha mabadiliko ya tabianchi, kwani zimekuwa zikizalisha hewa ukaa ambayo ndio chanzo cha ongezeko la joto, mafuriko, ukame, kuongezeka kwa kina cha bahari, vimbunga na majanga mengine.

Kauli hizo za kitaalamu zinaungwa mkono na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo anayesema ukataji miti ovyo ni moja ya vitu vinavyochangia uharibifu wa mazingira.

“Changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ni kubwa, imesababisha ukame na tunaona kwenye Wilaya za Longido, Kiteto na Simanjiro, mifugo inakufa kwa kukosa chakula, hali si nzuri kwenye wilaya hizi,” anasema.

Anaeleza maeneo kama Longido na Simanjiro ambayo yameathirika zaidi na ukame, kuna jamii kubwa ya wafugaji na uharibifu unapofanyika zaidi sehemu moja, hata maeneo mengine nchini yanaathirika.

“Uharibifu wa kimazingira unapofanyika, huathiri maeneo mengine pia hata theluji kwenye Mlima Kilimanjaro inayeyuka. Tanzania tumeandaa kanuni na muongozo katika kushughulika na hili, pia tunakwenda kushughulikia biashara ya hewa ya ukaa.

“Itakuwa ni fursa kwenye misitu, lakini pia wale wanaofanya kilimo cha mikorosho, parachichi na kahawa wataweza kushughulika pia na biashara ya hewa ya ukaa. Itasaidia wananchi kuwaza kutunza mazingira, mbali na miti lakini pia watapata faida ya hewa ukaa, watakapoharibu miti watakosa fursa ya fedha pia,” anasema.

Unachotakiwa kufanya katika biashara hii ni kuhifadhi misitu ya asili na mazingira. Misitu ya asili ina uwezo mkubwa wa kufyonza na kuhifadhi hewa ukaa na hewa.

Sumu

Baadhi wamenufaika na mpango huo unaoratibiwa na taasisi ya Carbon Tanzania kwa mujibu wa makala iliyochapishwa na gazeti la Serikali la Habari Leo Januari 5, 2021, wananchi 21,000 wa vijiji vinane kutoka Wilaya ya Tanganyika, Katavi wamelipwa Sh380 milioni kupitia Carbon Tanzania chini ya

mradi uitwao Ntakata Mountains Redd Plus Project.

Kwa mujibu wa makala hayo, “wananchi katika wilaya hiyo wamezuia uharibifu wa misitu waliyoihifadhi ili iwasaide kutunza mazingira ikiwamo kufyonza hewa ukaa na hewa sumu iliyo katika anga la nchi yetu na nje ya nchi.”

Makala hiyo inaeleza kutokana na uhifadhi huo, vijiji husika vimevuna jumla ya tani 82,000 za hewa ukaa na kuiuza kwa Sh250 milioni na kwamba pamoja na uvunaji wa tani hizo, mauzo yake hayajafikia hata nusu ya tani 270,000 ambazo bado hazijauzwa.

Waziri Jafo anasema bado uharibifu wa mazingira unafanyika nchini, hali inayosababisha ukame na athari nyinginezo ikiwamo ya vyanzo vya maji kupungua.

“Tunahitaji ushirikiano wa pamoja kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, wenzetu wa maliasili wana jukumu la kulinda na kuhifadhi misitu, basi wahakikishe inalindwa na kutunzwa, miti isikatwe ovyo.

“Tunashirikiana pia na wenzetu wa Wizara ya Maji kuhakikisha maeneo ya mabonde na vyanzo vya maji hayavamiwi na kuharibiwa, Wizara ya Nishati ifanye ubunifu jinsi gani tutapata nishati mbadala kwa bei nafuu, ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Anasema ushirikiano wa pamoja katika kutunza mazingira ndiyo njia pekee ya kukabiliana na ukame, akisisitiza kampeni ya kupanda miti milioni 1.5 kwenye kila halmashauri na milioni 276 kote nchini ambayo itachangia kupunguza changamoto hiyo.

Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Samwel Gwamaka anasema uharibifu wa mazingira umesababisha ikolojia nzima kuharibika.

Viko vitu vingi vimesababisha uharibifu wa mazingira, tumeona kule Kanda ya Ziwa ukataji miti ovyo umekithiri, wimbi hilo limeshuka hadi mikoa ya Lindi na Mtwara na sehemu nyingine nchini.

“Matumizi ya nishati na maendeleo ya viwanda yamesababisha kuzalishwa kwa kaboni, magari mengi yanatumia dizeli yanatoa moshi, vyote vinachangia uharibu wa mazingira,” anasema.

Dk Gwamaka anasema uchomaji moto pia unasababisha uharibifu, akitolea mfano tukio la karibuni la Mlima Kilimanjaro kuungua, lakini pia kusafisha mashamba kwa njia isiyo rasmi kwa kuchoma moto.

“Vyote hivyo vinaongeza kiwango cha hewa ukaa ambayo hubadili mwelekeo wa majira, zamani matukio ya mafuriko hayakuwepo, lakini sasa yanatokea kwa wingi sababu ya uharibifu, hakuna uoto, mvua ikinyesha haiingii ardhini kuweka akiba maji.

“Upandaji miti ambayo si rafiki inanyonya maji sana, misitu mingi ikiwamo ile ya miti ya mbao siku hizi hata nyani huwezi kumkuta, zamani waliishi humo, vinyesi vyao vilikuwa ndiyo mbolea, sasa uharibifu umekithiri na kusababisha ukame, kifupi ikolojia nzima imeharibika,” anasema.

Upande wa nishati

Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato anasema hali si nzuri kwenye vyanzo vya umeme, maji yanapungua kila siku kutokana na ukame.

Hali ya upungufu wa kina cha maji kwenye vyanzo vya umeme ni kubwa na kupungua huko kumesababisha kupungua Megawati 160 kwenye gridi ya taifa.

Anasema nishati za maji na gesi zote zinapaswa kupewa nguvu kubwa, ili kupata nishati ya uhakika kwa kuwa vyanzo vyote vinashirikiana.

“Lazima tuwe na energy (nishati) mchanganyiko. Tuwe na maji, gesi, upepo, jua na makaa ya mawe. Hizi ni njia tofauti za kupata nishati. Kwa mfano, sasa ukame umesababisha maji kupungua, hivyo tunatumia zaidi gesi, maji yakiwepo tunapunguza gesi tunatumia zaidi maji kwa kuwa tunayapata bure, gesi inanunuliwa.

“Huwezi kuweka nguvu kubwa kwenye gesi kwa kuwa ni gharama, lakini pia kwenye maji kwa kuwa kuna wakati yanapungua, hivyo tunatumia vyote.

“Tuna mradi wetu mkubwa wa Mwalimu Nyerere, ukikamilika utatupa Megawati 2,115, lakini bado wakati huohuo tunapata takribani Megawati 1,100 kutoka kwenye gesi kwa sasa, hivyo vyote vinashirikiana,” anasema.

Naibu waziri anasema jitihada zinafanyika, ili kutumia nishati ya makaa ya mawe ambayo hata hvyo, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la kufuatilia usimamizi wa rasilimali za asili (NRGI), Silas Osang anasema nishati hiyo ni changamoto kwani ni vigumu kupata uwekezaji kwenye kujenga vinu vya kuzalisha umeme,.

Lakini waziri anasema makaa ya mawe yataziba pengo la upungufu wa nishati akisisitiza kwamba Afrika haijachafua hali ya hewa kiasi kikubwa kama yalivyo mabara mengine.

“Wakati wazungu wanatumia makaa ya mawe sisi hatukuwepo huko, sasa tunataka kuanza kutumia wanatuzuia. Lakini vita ilipotokea Ukraine, Ujerumani imeagiza makaa ya mawe mara nane zaidi ya ilivyokuwa ikiagiza kutoka Afrika Kusini, wao wakikutwa na janga, makaa ya mawe hayachafui hali ya hewa lakini sisi tukitaka kutumia, makaa ya mawe yanachafua.

Hata hivyo, Osang anasema, “hii ni nishati chafu, nafikiri kwenye makaa ya mawe tumechelewa na fursa zimeshapita. Nishati ya uhakika ni maji au gesi. Vyanzo vyote viwili vina faida na changamoto zake, hasa nyakati hizi ambazo dunia inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.”

Nini kifanyike

Huko Zimbabwe, baada ya kumalizika kwa ukame uliokuwa na athari kubwa zaidi, kikao cha watafiti wa kimataifa kilianzisha mpango wa kupanda miti inayokua vizuri na haraka katika maeneo makavu. Lengo lilikuwa kukabiliana na changamoto ya nishati ya kupikia ambayo ilikuwa inategemewa kwa asilimia 80.

Hapa nchini kati ya mwaka 1988 na 2017, aliyekuwa mwenyekiti wa kampuni za IPP, Regnald Mengi alianzisha kampeni ya kupanda miti zaidi ya milioni 27 mkoani Kilimanjaro.

Utafiti wa “mtazamo wa sekta ya misitu 2020-2040” unabainisha kwamba kupunguza uzalishaji wa gesi ukaa kunategemea uwezo wa misitu kuchukua kaboni na kuongeza uzalishaji wa bidhaa mpya za kibunifu ambazo zinaweza kuchukua nafasi ya nyenzo zinazoingiza uzalishaji mkubwa zinazotumika katika ujenzi, nguo na uzalishaji wa nishati.

Kwa maana hiyo, wataalamu wengi wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi wanahimiza urejeshaji wa uoto wa asili kama njia sahihi na ya uhakika wa kukabiliana na hali ilivyo sasa.

Mifugo

Wakati ushauri ukiwa hivyo katika misitu, wafugaji nao wamekuwa wakihamasishwa kuchukua hatua mbalimbali, ili kujinasua katika janga la ukame ambalo linasababisha mifugo yao kukosa malisho na maji.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Jeremiah Wambura anasema mfugaji mmoja mwenye ng’ombe 450 anaweza kuvuna baadhi ya mifugo, ili kuhudumia wachache anaoweza kuwamudu.

“Tunatoa elimu kwa wafugaji kuuza baadhi ya mifugo, ili kupunguza mahitaji ya chakula. Lakini pesa hizo pia anaweza kuzitumia kujenga kisima cha maji kwa ajili ya mifugo yake,” anasema na kuongeza:

“Mvua zikianza kunyesha, nyasi nyingi zinaota, ni muhimu kuvuna nyasi na kuzihifadhi kwa ajili ya matumizi ya baadaye, kwa hiyo tunaendelea kuwaelimisha juu ya tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa.”

Maji

Mtaalamu wa maji kutoka Chuo cha Maji cha Dar es Salaam, Dk Adam Karia anasema kila inapofika kipindi cha ukame watu wengi wanainyooshea mkono Serikali, lakini wanasahau kwamba wangeweza kuepukana na kadhia hiyo kama wangeweka utaratibu wa kuhifadhi maji.

“Bado tunaweza kuvuna maji mengi katika ngazi ya kaya na yakahifadhiwa vizuri. Wataalamu wapo wa kuwafundisha namna nzuri ya kuyahifadhi,” anasema Dk Karia.

Mtaalamu huyo anabainisha kwamba changamoto nyingine ni elimu kuhusu matumizi bora ya maji, “unaweza kukuta mtu amesimama kwenye bomba anaacha maji yanatiririka wakati anapiga mswaki, akimaliza ndipo ananawa. Sasa hayo siyo matumizi sahihi ya maji. Tujifunze kutumia kidogo kinachokuwepo, ili tusiongeze uhitaji zaidi wa maji.”

Kuhusu miradi mikubwa ya pamoja, Dk Karia anasema Bwawa la Kidunda ambalo limezungumzwa kwa muda mrefu litakuwa suluhisho la kudumu la changamoto ya maji kwa sababu litahifadhi maji mengi ya mvua badala ya kuyaacha yakapotelea baharini.

“Mradi huu ni muhimu sana, utasaidia kufanya maji yapatikane muda wote kwa wananchi na kumaliza kero hizi tunazopitia sasa,” anasema Dk Karia.

Kuhusu mradi huo Waziri wa Maji, Jumaa Aweso anasema, “tulikuwa na mpango wa zaidi ya miaka 50 wa Bwawa la Kidunda, lakini tunashukuru Rais Samia Suluhu Hassan ametoa uamuzi kwamba lijengwe na mkandarasi tumeshampata. Hivi karibuni tutaanza finding ya mradi huo. Kwa hiyo hii itakuwa ndiyo suluhu kabisa ya tatizo la maji kwa jiji la Dar es Salaam na Pwani.”

Ujenzi wa visima katika ngazi ya kaya umefanikiwa baadhi ya maeneo kama vile Nanyamba, Nanyumbu, Newala na Tandahimba ambapo kila nyumba inayojengwa inakuwa ni mifumo ya kuhifadhi maji.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Nanyamba, Edwin Mwailafu anasema suala hilo ni utamaduni kwa wananchi wa Nanyamba kwa sababu wanajua hali halisi ya upatikanaji wa maji katika mazingira yao.

Anasema utamaduni huo umekuwa ukiwasaidia kuhifadhi maji ya mvua na yale ya bomba yanapotoka, jambo ambalo linawaongezea uhakika wa maji wakati wote. Anasisitiza kwamba jambo hilo si lazima, bali ni utamaduni ambao umekuwepo.

“Hili jambo siyo la lazima, lazima yetu ambayo tumeiweka na tunapiga faini ni kufunika kisima. Mtu akichimba kisima ni lazima akifunike, hili la kuchimba kisima siyo jambo la lazima kwamba asipofanya tutamtoza faini, hapana,” anasema mkurugenzi huyo.

Mwailafu anasema wanawahamasisha wananchi kujenga na kuhifadhi maji kwenye visima kwa sababu ni njia rahisi ambayo inawasaidia kipindi cha kiangazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live