RAIS John Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuzitumia mvua zinazonyesha nchini kote kulima kwa wingi mazao hasa ya chakula kwa kuwa yatahitajika kwenye nchi ambazo wananchi wake wamefungiwa kutokana na ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Rais Magufuli pia amewapongeza Watanzania kwa kuchapakazi na kulipa kodi inayotumika kutekeleza miradi ya maendeleo ukiwamo ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi.
Ametoa wito kwa kila Mtanzania kuhakikisha analipa kodi ipasavyo na kudai risiti kila anaponunua bidhaa au huduma.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa kwa vyombo vya habari jana ilieleza kuwa, Rais Magufuli aliyasema hayo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi.
Daraja hilo litakuwa na urefu wa kilometa 3.2 na hivyo kuwa refu zaidi Afrika Mashariki na Kati.
Linajengwa na mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kwa gharama ya takribani Sh bilioni 700 na linatarajiwa kukamilika Februari 2024.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Vedastus Maribe alimweleza Rais Magufuli kuwa ujenzi wa daraja hilo ulianza Februari 25 mwaka huu.
Alisema ujenzi huo umefikia asilimia 11.18 ikiwamo ujenzi wa daraja la muda ambalo limefikia asilimia 51.6 na kwamba hadi kukamilika kwake linatarajiwa kuwa na nguzo 67 zikiwamo tatu kubwa.
Akizungumza baada ya kuona kazi ya uchimbaji wa mashimo yenye urefu wa mita tatu ndani ya mwamba kwa ajili ya ujenzi wa nguzo hizo, Rais Magufuli alieleza kufurahishwa na hatua iliyofikiwa lakini akamtaka mkandarasi CCECC kuongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili likamilike haraka.
Rais Magufuli alisema daraja hilo lina umuhimu mkubwa kwa Watanzania na nchi jirani za Uganda, Burundi, Rwanda na DRC, pia akasimulia mkasa uliosababisha aweke dhamira ya kuhakikisha linajengwa.
Alisema yeye ni mmoja wa walionusurika kufa maji baada ya mtumbwi aliokataa kuupanda kuzama na kusababisha vifo vya watu 11 waliokubali kuupanda ili kuvuka kutoka Busisi kwenda Kigongo.
Aliwapongeza wananchi wa Kanda ya Ziwa kwa kujengwa kwa daraja hilo ambalo litaepusha ajali za mara kwa mara za kuzama kwa mitumbwi inayovusha watu na bidhaa kati ya Kigongo na Busisi.
Alitoa wito kwa wananchi hasa vijana wanaopata ajira katika mradi huo kufanya kazi kwa bidii na uadilifu badala ya kuiba vifaa vya ujenzi.