Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JICA, Serikali kuboresha usafiri wa reli Dar

TRL TRENI JICA, Serikali kuboresha usafiri wa reli Dar

Tue, 9 Nov 2021 Chanzo: ippmedia.com

Shirika la Maendeleo la Japan JICA, Wizara ya ujenzi na Uchukuzi pamoja na Shirika la Reli Tanzania wamekubaliana kutekeleza mradi wa utafiti wa ukusanyaji wa taarifa na uboreshaji wa huduma ya usafiri wa reli jijini Dar es Salaam kuanzia mwezi huu wa Novemba 2021.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa JICA Tanzania, Henry Kajange, utekelezaji wa mradi huo utafanyika kwa kipindi cha miezi minne na unatarajia kukamilika Februari mwaka 2022.Kajange alisema maeneo ya utafiti na kukusanya taarifa ni miundombinu ya reli za abiria Pugu na Ubungo.

Alisema baada ya kazi hiyo kukamilika, timu iliyoundwa itatoa mapendekezo kwa ajili ya hatua mbalimbali za maboresho yake.Alisema lengo ni kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam na kupunguza tatizo la msongamano.

“Katika mkutano wa kwanza ulioketi Novemba 4, mwaka huu, washirika wa mradi huo walipendekeza mpango wa uboreshaji wa ufuatiliaji wa uendeshaji wa reli, uwekaji ishara, usafirishaji wa bidhaa, ujenzi wa stesheni katika vituo, majengo ya biashara katika stesheni na namna bora ya kutoa huduma ya usafiri katika njia za treni za abiria zilizopo,” alisema Kajange.

“Timu ya watafiti iliyoundwa, itajadiliana na maofisa wa Serikali ya Tanzania, ili kurekebisha mpango wa usafiri wa mijini wa Dar es Salaam wa mwaka 2018, uliofadhiliwa na JICA. Mpango huo ambao unakadiria kwamba jiji hilo litakuwa na zaidi ya watu milioni 10 ifikapo mwaka 2030, usafiri wa barabara pekee hautaweza kutoa uhakika na kuondoa kero ya msongamano wa magari na kutumia muda mrefu wa kusafiri ndani ya jiji hilo.”

Jingine ni kupendekeza katika mkutano huo namna bora ya uboreshaji wa mfumo wa reli uliopo, kwa ajili ya maendeleo ya usafiri na mipangilio mizuri yenye uwiano.Kwa mujibu wa Kajange, JICA inasaidia sekta ya uchukuzi kwa zaidi ya miaka 40, nchini Tanzania.

Chanzo: ippmedia.com