Baada ya mamlaka nchini Kenya kutoipa vibali vyote vya uwekezaji kampuni ya Taifa Gas kujenga kiwanda cha gesi ya kupikia Bandari ya Mombasa, mmiliki wa kampuni hiyo, Rostam Aziz amesema wanafuatilia kupata kila kinachohitajika, ili uwekezaji huo uendelee kama ulivyopangwa.
Rostam alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akithibitisha kupata taarifa za kwenye mitandao ya kijamii ya kuzuiwa kwa kampuni yake kuendelea na uwekezaji iliyouomba.
Hata hivyo, alikiri hajapata barua yoyote kutoka mamlaka za nchi hiyo jirani ambayo ni mwanachama mwenza wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Taifa Gas inaendelea kufuatilia vibali vya mradi huu ikiongozwa na Mamlaka ya (Maeneo Maalumu ya Uwekezaji) SEZA kwa mujibu wa sheria za uwekezaji za Kenya,” alisema Rostam.
Msimamo huo wa Rostam unatokana na taarifa iliyoripotiwa juzi na gazeti la Business Daily la nchini Kenya kwamba, mamlaka nchini humo zimeukataa mradi huo kutokana na kutishia usalama wa mazingira.
“Hatujaridhia na kuidhinisha ripoti yao ya tathmini ya Mazingira na Madhara kwa Jamii (ESIA) kutokana na upungufu wa kiufundi tuliouona. Tathmini ya mazingira ilikuwa na kasoro zinazopaswa kurekebishwa kabla hatujawaruhusu waendelee na hatua zinazofuata,” ilisema EPRA ilipojibu maswali yaliyoulizwa na gazeti la Business Daily.
Mamlaka hiyo haikubainisha kasoro hizo za kiufundi ambazo Taifa Gas inayotaka kupata sehemu ya soko la kaya milioni 2.87 zinazopikia gesi, ambazo ni sawa na asilimia 23.9 ya kaya zote nchini Kenya, inatakiwa kuzirekebisha.
“Taifa Gas imeona taarifa za mradi wake wa uwekezaji Kenya kukataliwa na EPRA kwenye mitandao ya kijamii leo (jana) asubuhi tarehe 21/07/2022,” alisema Rostam.
Taifa Gas inakusudia kujenga mtambo wa tani 30,000 katika eneo maalumu la uwekezaji Dongo Kundu jirani na Bandari ya Mombasa, hivyo kuongeza ushindani kwa kampuni za Vivo, Rubis na Total pamoja na Africa Gas and Oil Limited (AGOL) zinazosambaza nishati hiyo nchini humo.
Iwapo Taifa Gas itakamilisha uwekezaji, itakuwa kampuni kubwa zaidi nchini humo kwa kuizidi AGOL inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu, Mohamed Jaffer.