Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Iran yabainisha fursa za uwekezaji Tanzania

Iran Iran Irannn.jpeg Iran yabainisha fursa za uwekezaji Tanzania

Sat, 10 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar es Salaam. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeelezea matarajio yake ya kuongezeka kwa kiwango cha biashara kati yake na Tanzania, huku ikiahidi kuchukua kila hatua kufanikisha hilo na kubainisha maeneo muhimu yenye fursa za kiuwekezaji

Matarajio na ahadi hiyo imetolewa Februari 9,2024 na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Hossein Alvandi Vehineh wakati wa maadhimisho ya miaka 45 ya Mapinduzi ya Iran, ya mwaka 1979, yaliyouondoa utawala wa kifalme na kusimika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika katika makazi ya Balozi, jijini Dar es Salaam, Balozi Vehineh amesema kuwa mwaka uliopita kiwango cha biashara kati ya nchi hizo kilikuwa Dola za Marekani 60 milioni (Sh150.3 bilioni).

Amefafanua kuwa Iran iliingiza nchini bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 40 (Sh100.2 bilioni), huku ikiagiza bidhaa kutoka Tanzania zenye thamani ya Dola milioni 20 (Sh50.1 bilioni) tu.

Hata hivyo, amesema kutokana na hatua zinazochukuliwa za kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande zote, wanatarajia kuwa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kitaongezeka katika siku chache zijazo.

Amesema kuwa bado kuna maeneo muhimu ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili yakiwamo ya kilimo, migodi, uvuvi, ufugaji na sayansi na teknolojia.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Omar Said Shaaban, ametoa wito kwa pande zote kuongeza juhudi kuimarisha ushirikiano katika eneo hilo la biashara na uwekezaji.

Amebainisha kuwa Tanzania chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa ni Taifa la kwanza la Kiafrika kuipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Mapinduzi ya mwaka 1979, kuanzia hapo uhusiano na ushirikiano huo umeendelea kukua siku hadi siku katika sekta mbalimbali.

Hata hivyo, amesema kuwa kiwango cha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, kwa hivi karibuni kimepungua sana.

“Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Viwango (TBS), kiwango cha uwekezaji na biashara kati ya nchi hizo mbili kimepungua kutoka Dola 18.8 milioni (Sh 47 bilioni) mwaka 2017 mpaka Dola 2.8 milioni (Sh7 bilioni) mwaka 2022,” amesema Shaaban.

Kutokana na takwimu hizo, Shaaban amesema kuwa zinahitajika juhudi za pamoja kuimarisha biashara, uwekezaji na utalii kwa manufaa ya nchi zote mbili na watu wake.

Katika nyanja ya uwekezaji amesema kuwa Kituo cha Uwekezaji (TIC) kumbukumbu zinaonyesha kuwa kuna kampuni 15 za Iran za uwekezaji zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 333.23.

Hata hivyo, amesema jukwaa la biashara na uwekezaji la mwaka 2022 lililofanyika jijini Dar es Salaam limefungua milango kwa wawekezaji wa Iran kuwekeza nchini.

"Oktoba 2023 Tanzania ilipokea uwakilishi wa wafanyabiashara kutoka kampuni 10 za Iran ambazo zilikuja kuangalia uwezekano wa kuwekeza na kufanya biashara na kampuni za Tanzania katika sekta ya nyama na wanyama walio hai, kemikali za viwandani, uvuvi wa baharini, migodi na afya,” amesema.

Amezishukuru kampuni hizo kwa kuonyesha nia ya kununua nyama na wanyama hai kutoka Tanzania, akisema kuwa huo ni uamuzi usio na shaka kwani Tanzania ni sehemu sahihi.

"Tanzania ina idadi kubwa ya mifugo bora inayojumuisha ng'ombe 25.8 milioni, mbuzi 16.7 milioni, kondoo 8.7 milioni.”

“Ngoja nikuhakikishie Balozi, hii idadi kubwa ya wanyama ni kuonyesha utayari wa Tanzania kulisha soko linalokuwa la Iran nyama safi na bora na wanyama hai. Balozi hebu tulifanyie kazi kwa pamoja eneo hili,”ametoa rai Shaaban.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live