Dar es Salaam. Uongozi wa kampuni ya Said Salim Bakhresa & Ltd (SSB) umewatahadharisha baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia vifungashio vilivyotumika katika bidhaa za Azam na kujaza bidhaa nyingine zenye mwonekano wa kampuni hiyo na kuziuza wa wateja.
Wameeleza hayo leo Jumanne Septemba 3, 2019 na uongozi wa kampuni hiyo ya kutengeneza vyakula inayomilikiwa na kampuni (SSB) kupitia kwa mkurugenzi wa uhusiano wa SSB, Hussein Sufian.
Sufian amesema wamebaini uwepo wa baadhi ya wazalishaji wenye tabia ya kuiga na kubadilisha rangi na mwonekanao wa bidhaa za Azam kila wanapofanya mabadiliko ya bidhaa zao mbalimbali.
"Kufanya hivi ni kosa la kisheria tayari tumeshatoa taarifa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kulifanyia kazi ili wale wote wanaojihusisha na tabia hii wachukuliwe hatua za kisheria," amesema Sufian.
Sufian ameeleza kuwa katika kukabiliana na hali hiyo, uongozi wa kampuni hiyo umeamua kubadilisha mwonekano wa bidhaa yake maarufu ya unga wa ngano unaoitwa ngano bora.