Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ilala yaongoza ugawaji wa vitambulisho Dar es Salaam

31446 Vitambulisho+pic TanzaniaWeb

Thu, 13 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ikiwa ni siku ya pili tangu kuanza kugawiwa kwa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo maarufu machinga, tayari Wilaya ya Ilala imeuza takriban theluthi mbili ya idadi iliyopewa na uongozi wa mkoa.

Rais John Magufuli alitoa vitambulisho 25,000 kila mkoa kwa ajili ya wafanyabiashara hao, ambao mapato yao hayazidi Sh4 milioni kwa mwaka, akitaka wasibughudhiwa baada ya kulipia Sh20,000.

Mkoa wa Dar es Salaam, ambao una wilaya tano, umegawa vitambulisho 5,000 kila wilaya.

Lakini ni wilaya tatu tu ambazo zilikuwa zimeanza kuwagawia wafanyabiashara hao vitambulisho hivyo, huku Ilala ikiwa imeshakabidhi zaidi ya wafanyabiashara 3,000 hadi jana saa 7:00 mchana.

“Mwitikio wa machinga katika wilaya yetu ni mkubwa pengine ni kwa kuwa kwa siku nyingi walikuwa wanasumbuliwa na mgambo katika biashara zao,” alisema katibu tawala wa wilaya, Sheilla Lukuba.

“Tayari tumeuza zaidi ya vitambulisho 3,000 katika eneo hili. Mpango wa baadaye ni kwenda kata kwa kata.”

Lukuba alisema wanaopewa vitambulisho sasa ni ambao walikuwa katika kanzidata za manispaa ya wilaya hiyo, wasiokuwamo taarifa zao zitachukuliwa kwa ajili ya kuthibitisha kama wanastahili.

Naye katibu tawala Wilaya ya Kinondoni, Stella Msofe alisema kazi hiyo ilianza juzi na hadi jana saa 5:00 asubuhi walikuwa wametoa vitambulisho kwa watu 315.

“Vitambulisho vyetu tunagawia hapa Mwenge kwa kuwa ndiyo centre (katikati), lakini tutahamia maeneo mengine,” alisema Msofe.

“Tunatumia kanzidata yetu ya wamachinga. Wale ambao hawapo kwenye mfumo kuna utaratibu wa kujiandikisha kwanza.”

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo wa soko la Mwenge, Omary Khamis aliibua hoja ya kutaka Serikali iangalie namna ya kuwashughulikia watu wanaofanya biashara ya machinga na maduka kwa wakati mmoja.

Hata hivyo, Msofe alisema vitambulisho hivyo vitatolewa kwa machinga tu.

Katika wilaya ya Ubungo, vitambulisho vilianza kutolewa jana mchana huku mkuu wa wilaya hiyo, Kisare Makori akizindua kazi hiyo katika soko la wafanyabiashara la Simu 2000.

Kisare aliwataka wafanyabiashara hao kuwa makini na matumizi ya kitambulisho na wasikubali kutumiwa kuuza bidhaa za wafanyabiashara wakubwa wanaokwepa kodi.

Tukikubaini tunakunyang’anya kwa sababu utakuwa umekwenda kinyume na matumizi ya vitambulisho hiki,” alisema Kisare katika uzinduzi huo.



Chanzo: mwananchi.co.tz