Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ifahamu Taasisi mpya ya TOSS

Tax Tax Ushuruuuu Ifahamu Taasisi mpya ya TOSS

Mon, 11 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ili kumaliza migogoro ya kikodi iliyopo baina ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na walipakodi, Serikali imeanzisha Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi Tanzania (TOST).

Katika taasisi hiyo, mlalamikaji hatalazimika kuwa na uwakilishi wa mwanasheria ili awasilishe malalamiko, badala yake anaruhusiwa kupeleka mwenyewe.

Hata hivyo, taasisi hiyo imeanzishwa kipindi ambacho kumekuwa na malalamiko katika utekelezwaji wa sheria za kikodi.

Miongoni mwa yanayolalamikiwa ni TRA kutumia nguvu, kufunga biashara na wakati mwingine kukadiria kodi isiyolingana na thamani ya biashara iliyofanyika.

Taarifa kuhusu kuanzishwa kwa TOST, imetolewa jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Desemba 11, 2023 na mkurugenzi wa taasisi hiyo, Robert Manyama mbele ya wahariri na waandishi wa habari.

Amesema lengo la kuanzishwa kwake ni kushughulikia malalamiko yatokanayo na usimamizi wa sheria za kodi kwa kuzingatia uhuru katika utendaji, ufanisi, uwazi, uhalisia na haki.

Lengo lingine, amesema ni kuainisha maeneo yenye matatizo katika usimamizi wa sheria za kodi ambayo ni vyanzo vya malalamiko na kutoa mapendekezo ya marekebisho.

"Madhumuni mengine ni kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani na kuongeza imani kwa wananchi na ulipaji wa kodi wa hiari," amesema.

Manyama amesema mtu yeyote anayeona kutoridhishwa na utendaji wa mamlaka inayosimamia utekelezaji wa sheria ya kodi, anaweza kuwasilisha malalamiko yake.

Kulingana na Mkurugenzi huyo, malalamiko hayo yanaweza kuhusu TRA, Kamishna wa TRA au hata mtendaji yeyote wa mamlaka hiyo.

Kuhusu namna yanavyoshughulikiwa, Manyama amesema baada ya lalamiko kuwasilishwa kwa mujibu wa sheria linapaswa kusuluhishwa ndani ya siku 30.

“Malalamiko yanapaswa kuwasilishwa ndani ya siku 90 tangu yalipotokea na kama usuluhishi wake utahitaji marekebisho tutayapendekeza na kuwasilisha kwa Waziri wa Fedha," amesema.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Hamis Livembe amesema tatizo kubwa la sasa ni utaratibu uliopo.

Kabla ya kuanzishwa kwa TOST, amesema TRA ikimkadiria mfanyabiashara kodi hana pa kwenda kulalamika hata ikiwa kinyume na uhalisia.

"Rufaa inakatwa kwa Kamishna wa TRA, yaani huyo huyo aliyekukadiria ndiye unayekwenda kukata rufaa kwake.

"Na ili usikilizwe unapaswa ufanye malipo ya awali theluthi moja ya fedha ulizokadiriwa, ambazo wakati mwingine uhalisia wa kodi unayodaiwa haifiki hata kiwango hicho," amesema.

Amesema uwepo wa TOST unawapa wafanyabiashara jukwaa la kwenda kulalamika, ingawa bado walipakodi wana wasiwasi.

Wasiwasi walionao, amesema ni taasisi hiyo kuwa chini ya Wizara ya Fedha, ambayo pia ndiyo mlezi wa TRA.

"Sasa wakienda kuwa watoto wa baba mmoja yaani waziri anayeisimamia TRA na TOST ni mmoja, huenda wakawa washirika, ndiyo wasiwasi wa walipakodi lakini tutaona kwenye utendaji wao," amesema.

Hata hivyo, amesema Desemba 15, mwaka huu amealikwa kushiriki uzinduzi wa taasisi hiyo, jukwaa wanalotarajia kulitumia kuuliza maswali na kupata taarifa zaidi kuhusu TOST.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live