Shirika la kazi duniani (ILO) limetaka kuchukuliwa kwa hatua za ziada kushughulikia, kuhifadhi kemikali pamoja na utolewaji wa mafunzo kwa wafanyakazi wa bohari za kemikali, ili kuepusha mfanano wa janga lililotokea kwenye bohari ya kontena mjini Chattogram kusini mashariki mwa Bangladesh.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jijini Dhaka nchini humo, inasema tukio hilo limedhihirisha umuhimu wa mafunzo ya jinsi ya kudhibiti msongamano wa watu wakati wa janga kama hilo litakalosaidia kuokoa vifo, mali na uharibifu wa miundombinu.
Katika tukio, hilo inadaiwa kuwa askari wa kikosi cha zimamoto walishindwa kuuzima moto huo ulioanza majira ya usiku usiku wa Juni 5, 2022 katika eneo la Dutch lililo umbali wa kilometa 216 kusini mashariki mwa mji mkuu wa nchi hiyo Dhaka.
Mbali na ILO kutuma salamu za rambirambi kwa familia za watu waliopoteza maisha sambamba na kuonesha mshikamano kwa familia za waliojeruhiwa, pia imetaka kuimarishwa kwa mifumo ya usalama, kuzingatia utoaji mafunzo ya usalama na ushughulikiaji wa majanga maeneo ya kazi.
Maeneo makuu ambayo ILO inatilia mkazo ni kuangaliwa upya kwa kanuni za usafirishaji na usimamizi wa vifaa, malipo ya kutosha ya fidia kwa majeruhi wa ajali kazini na usaidizi kwa wafanyakazi walioachwa na ulemavu baada ya ajali za aina hiyo na usaidizi huo ufikishwe pia kwa familia.
Tayari serikali ya Bangladesh, waajiri na vyama vya wafanyakazi nchini humo wamekubaliana kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa malipo ya ajali kazini, wakianzia na sekta ya ushonaji wa nguo (RMG), na kuna uwezekano wa kupanua mfumo huo kwa sekta nyingine.
Mfumo huo unatajwa kuhusisha kinga dhidi ya ajali, malipo ya fidia papo kwa papo na kwa muda mrefu na matibabu kwa mfanyakazi ili aweze kurejea kazini baada ya ajali.
Vyombo vya habari bado vinaripoti tukio la moto mkubwa unaoshukiwa kusababishwa na milipuko wa kemikali kwenye bohari ya kontena inayomilikiwa na kampuni ya BM yenye ubia kati ya Bangladesh na Uholanzi, uliosababisha vifo vya watu 49 wakiwemo wahudumu wa zimamoto na na mamia ya watu kujeruhiwa.