Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) umesema mpango mkakati wa kuboresha chuo hicho umewezesha kukusanya Sh26 bilioni ambayo inatokana na ongezeko la Sh15 bilioni la mwaka 2021/22 na hiyo inatokana na ongezeko la wanachuo.
Mkuu wa chuo hicho Profesa Eliamani Sedoyoka ameyasema hayo alipokuwa akizindua ripoti ya chuo hicho na kuyataja mafanikio hayo yametokana na ongezeko la wanachuo ambapo kwa sasa wapo 13,716.
Ametaja mengine kuwa ni pamoja na kujengwa kituo kikubwa cha habari na mawasiliano kwa nchi za Afrika (ICT) ambacho kitaanza mwakani na kutekeleza miradi ya ujenzi wa hosteli za wanachuo.
“Mafanikio mengine ni kujengwa kwa matawi ya chuo hicho katika mikoa ya Dodoma, Babati na Ruvuma huku wakiendelea na ujenzi wa tawi la Ruvuma, kusomesha wahadhiri na watumishi wa kada zingine, kutoa mafunzo ya uhasibu na mafunzo ya mbinu za kisasa za ulinzi wa nchi kupitia mtandao (Cyber security) kwa maofisa wa Jeshi la Polisi yatakayotolewa kupitia chuo cha Polisi Moshi,” amesema Profesa Sedoyoka
Amesema chuo hicho katika mafanikio hayo kinasomesha wahadhiri 65 wa ngazi mbalimbali lengo ni watumishi wote wafikie madaraka ya juu ya elimu, kuimarisha mkakati wa kusimamia na kuendeleza vyanzo vya mapato hayatokani na ada za wanachuo pia lengo ikiwa ni kuboresha mapato ya chuo.
Profesa Sedoyeka ametaja mengine ni kuendesha chuo kwa mfumo wa kuwepo idara za chuo na badala yake kuwepo na mfumo wa kurugenzi ambao umekuwa na manufaa makubwa katika uendeshaji wa chuo.
“Chuo kinatoa mafunzo ya ulinzi wa nchi kwa kutumia mtandao kwa Jeshi la Polisi ili kuwawawezesha kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu ambapo masomo hayo yanatolewa kwa maafisa wa polisi wenye shahada kupitia Chuo cha Polisi Moshi (CCP),” amesema
Aidha amesema chuo kinaendeleza mahusiano na Jeshi la wananchi (JWTZ), Jeshi la Polisi na lengo ni kuwezesha vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama kupata mafunzo mbalimbali chuoni hapo.