Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huu ndio utaratibu kusafirisha bidhaa zako nje kupitia bandari

2c5174c77c57963db600ad0f1cf72e51 Huu ndio utaratibu kusafirisha bidhaa zako nje kupitia bandari

Tue, 13 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaendelea kukuletea makala mfululizo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa katika bandari zake ili wewe mtumiaji na mwananchi uweze kuelewa kwa upana kazi zinazofanywa na TPA na majukumu yake katika kuhudumia shehena mbalimbali.

Kwanza kabisa, leo tunatoka na makala haya wakati TPA ikiwa na mkurugenzi mpya, Eric Hamissi, aliyeapishwa hivi karibuni kuchukua jukumu zoto la kuongoza bandari zetu ambazo ni muhimili muhimu wa maendeleo yetu.

Kabla ya uteuzi wake, Hamissi alikuwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (MSCL) ambayo ina jukumu la kusafirisha mizigo na abiria katika maziwa ya Victoria, Nyasa na Tanganyika.

Katika makala ziijazo tutaangalia hatua ambazo mtu anayeagiza mzigo anapaswa kuzifuata ili aweze kuupata mzigo wake kutoka bandarini.

Lakini katika makala ya leo tutaona hatua za usafirishaji mzigo kwenda ng’ambo kupitia bandarini, kuanzia kupata vibali, ukaguzi, kulipia na hatimaye kusafirisha.

Tafuta wakala wa forodha

Hatua ya kwanza ambayo msafirishaji anatakiwa kuichukua baada ya kupata soko la bidhaa zake nje ni kumpata wakala wa forodha kutoka ofisi za Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFFA).

Ni vyema ikaeleweka kwamba Bandari inafanya kazi na mawakala ili kurahisha utendaji na siyo msafirishaji au muagiza mzigo mmoja mmoja.

Njia rahisi ya kupata mawakala hawa ni kupitia katika tovuti yao na ile ya TRA. Huyu ndiye mtu ambaye atamsaidia msafirishaji kuhakikisha mzigo wake husika unapitia hatua zinazotakiwa mpaka kuusafirisha.

Pia wakala anatakiwa amsaidie mwenye mzigo kupata vibali (export permits) vyote kutoka katika mamlaka husika kulingana na aina ya mzigo wake anaousafirisha.

Baada ya kupata kibali cha kusafirisha, wakala anatakiwa kupata nyaraka ya kuchukulia kontena kutoka kwa wakala wa meli (shipping agent) ambapo atapata gharama za kusafirisha mzigo (freight charges).

Katika hatua hii, wakala atapatiwa nyaraka ya kusafirishia mzigo ambayo inaitwa shipping order. Nyaraka hii inayotengenezwa na mteja akishirikiana na wakala wake ili kumsaidia kuitumia wakati wa kutoa taarifa za mzigo kwenye Mfumo wa Pamoja wa Forodha Tanzania uliochini ya TRA wa Tancis unaofanya kazi kwa njia ya kielektroniki.

Mfumo wa TANCIS unaisaidia TRA kurahisisha shughuli za forodha, unaongeza tija ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato ya serikali.

Utayarishaji wa mzigo na malipo

Hatua inayofuata ni wakala kuchagua eneo maalumu kwa ajili ya kupakia mzigo kwenye kontena chini ya uangalizi wa ofisa wa TRA ambaye atakagua mzigo pamoja na mamlaka zingine za vibali.

Kwa mfano, kama ni mzigo unaohusisha kemikali, lazima taasisi za kiserikali zinazohusisha masuala hayo ziwepo pia.

Baada ya kufanyika kwa ukaguzi, ofisa huyo atafunga kontena kwa kutumia lakiri (seal) ambayo ina namba maalumu, pia wakala wa meli naye atafunga seal yenye nembo au alama ya kampuni yake ya meli.

Wakala akishakamilisha hatua hiyo, atatakiwa kuingia kwenye mfumo wa TRA wa Tancis ili kuingiza taarifa za mzigo wa mteja wake na atapata nyaraka inayoitwa Tansad na nyaraka inayomruhusu kusafirishia mzigo (Release order).

Tansad in nyaraka yenye taarifa za usafirishaji mzigo (shipping order), orodha ya upakiaji vitu kwenye kontena (packing list), na stakabadhi ya malipo.

Baada ya kupata vibali vya TRA, wakala wa forodha atatakiwa kuviwasilisha TPA kwa Ofisa anayehusika ambaye ataingiza taarifa za mzigo kwenye mfumo wa TPA unaohusika na mizigo (cargo system).

Hatua hiyo itamwezesha wakala kuingia kwenye mfumo wa malipo wa TPA (e-payment system) ambapo atapata namba ya kumbukumbu ya kulipia tozo za TPA (payment reference number – PRN) kupitia benki mojawapo kati ya TIB, NMB, CRDB na Standard Charted au kwa njia ya mtandao wa simu.

Kuingiza mzigo bandarini

Wakala akishakamilisha malipo ya TPA, ataingia kwenye mfumo wa TPA ili kutoa taarifa za mzigo ili aweze kuingiza taarifa za gari na dereva kwa ajili ya kuingiza mzigo husika bandarini.

Taarifa atakazoingiza kwenye mfumo wa TPA ni pamoja na namba za lori litakaloleta mzigo bandarini, namba za kontena, jina la dereva na namba ya leseni ya dereva.

Baada ya kuingiza taarifa hizo kwenye mtandao wa TPA, wakala atapatiwa kibali kwa ajili ya kuingiza kontena bandarini. Kontena baada ya kufikishwa bandarini litapakiwa kwenye meli ili kusafirishwa kwenda ng’ambo.

Utayarishaji wa Bill of Lading

Bill of lading ni nyaraka yenye taarifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na jina na anuani ya muuzaji/msafirishaji wa mzigo, jina la nchi ulikonunuliwa mzigo, aina ya mzigo, namba za kontena lililopakiwa mzigo, jina la bandari lilikopakiwa kontena, jina la meli iliyochukua kontena, jina la aliyenunua mzigo na anuani yake na jina la bandari ambako kontena litakakoteremshwa.

Hivyo, mara tu baada ya kupakia kontena kwenye meli na meli kuondoka kutoka bandarini, wakala wa forodha kwa kushirikiana na wakala wa meli, wataandaa bill of lading na kuituma kwa mteja aliyenunua mzigo kule unakokwenda.

Ni muhimu sana kuzielewa hatua hizi za usafirishaji wa mizigo kwenda ng’ambo hasa kwa wakati huu ambao Tanzania ipo kwenye mapinduzi makubwa ya uchumi yaliyosaidia kuiingia nchi ytu kwenye uchumi wa kati hata kablayamuda uliotarajiwa.

Ni kipindi pia ambacho Tanzania imejikita katika kuleta uchumi unaotegemea viwanda.

Kwa kuwa uzalishaji bidhaa katika viwanda utalenga soko la nje pia, ni vizuri kwa wazalishaji wa bidhaa za viwandani, kwanza wakajikita vilivyo katika kutafuta soko la bidhaa zao nje na kisha kuzielewa hatua hizi ili kuwawezesha kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz